WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atamwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda iwapo hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya
dawa za kulevya, aina ya shisha.
Hatua hiyo inatokana na kauli ya Makonda kuwatuhumu Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda,
kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa
na watu waliotaka kumhonga lakini akakataa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa
Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema katika udhibiti wa suala la shisha, mkuu huyo wa mkoa amefanya
kazi nzuri, na kwamba kwa kuwa ameshatoa maelekezo, akiwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Makonda hana budi kuyatekeleza.
Alisema alivyosikia anawaagiza wakuu wake wa wilaya wote kusimamia
maagizo yake na kama hawakusimamia atachukua hatua, basi naye atachukua
hatua kwake (Makonda) asipotekeleza suala hilo ambalo kwa Mkoa wa Dar es
Salaam ni tatizo kubwa.
“Sasa mimi nasema nakuagiza wewe usimamie na kama hutasimamia suala hilo
nitakuchukulia hatua, hivyo hangaika na shisha kwa wanaopuliza wakiwa
wamelala hakikisha unawadhibiti,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa wakati
akijibu sehemu ya salamu za Makonda alipopewa fursa ya kusalimia
wananchi katika hafla hiyo.
Katika salamu zake, Makonda alisema Waziri Mkuu alipiga marufuku
matumizi ya shisha, hivyo alimwagiza Kamanda Sirro kuhakikisha suala
hilo linatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
“Lakini Waziri Mkuu nimeshangaa kupita katika baadhi ya maeneo na kuona
watu wameanza tena kuvuta shisha na nilipouliza wakasema wewe ndiyo
umetoa kibali cha shisha,” alieleza Makonda na kuongeza alishangaa
Waziri Mkuu alipiga marufuku shisha, ni lini ametoa kibali kuanza
kutumika.
Lakini mkuu huyo wa mkoa alienda mbali zaidi na kudai kuna kikundi cha
watu 10 waliokwenda kwake ambao anawatambua kama “maajenti wa shetani”
ambao wanapata faida kati ya Sh milioni 35 mpaka Sh milioni 45 kwa mwezi
kutokana na dawa hizo za kulevya.
Alidai watu hao walipanga mikakati ya kumshawishi kupokea Sh milioni
tano kwa kila mmoja kwa mwezi yaani Sh milioni 50 ili asipige kelele
kuhusu shisha na wao waendelee kupata faida.
“Shisha imerudi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nimeshamuagiza
Kamishna Sirro, lakini nimeona kama ana kigugumizi… lakini sijajua kama
hizi tano tano zimepita kwake na pia RPC wa Kinondoni nimemuona hapa,
lakini hawa wana kigugumizi sijui kama hizi tano tano zimepita kwao,” alisema Makonda.
Alisema aliamua kufanya ziara mwenyewe na kushuhudia watoto wadogo
wanavuta shisha, hivyo uwezekano miaka 10 ijayo vijana wengi kuwa
matatizo ya afya, hivyo kumwomba Waziri Mkuu kutochoka kusimamia suala
hilo na taasisi zote ili likome katika mikoa yote.
Kuhusu
wafanyabiashara wadogo, alisema suala hilo linamnyima usingizi na kutoa
rai kwa wakuu wa wilaya kuwa, kama kuna mkuu wa wilaya atachelewa
kutekeleza yale aliyoagiza kuwapeleka machinga katika maeneo
yaliyoruhusiwa atachukua hatua kabla ya Waziri Mkuu kufanya hivyo.
Aidha, alishukuru kwa mradi wa umeme akisema ukatikaji umeme una madhara
sana na hasa kwa wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na biashara
ndogo kama saluni na shughuli nyingine ndogo zinazojenga uchumi wa kati.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA