Dar es Salaam. Baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
(KUB), Freeman Mbowe kuibua tuhuma dhidi ya wabunge wa CCM akidai
wamepewa Sh10 milioni kila mmoja ili wapitishe mpango wa maendeleo ya
Taifa na muswada wa Sheria za Huduma za Habari, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa imeanza uchunguzi.
Takukuru imeanza kuchunguza tuhuma hizo siku chache baada ya Mbowe
kuziibua alipokuwa akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
bungeni mjini Dodoma.
Hata hivyo, swali hilo halikujibiwa na Waziri Mkuu baada ya Naibu Spika,
Dk Tulia Ackson kumkingia kifua akidai swali hilo halikuwa la kisera.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola amesema wameanza kufanya
uchunguzi juu ya suala hilo kwa sababu ni jukumu lao na watalifanya
kiuhakika.
“Kama Rais amesema tunachunguza suala hilo mnataka mimi niseme nini?
Ndiyo, tumeanza kuchunguza, Takukuru ni chombo chake na tumeanza kazi
hiyo. Kama na wewe una ushahidi tuletee tuufanyie kazi,” amesema Mlowola
alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wetu juu ya suala
hilo.
Alipoulizwa kama analifanyia kazi suala hilo, Kamishna Mkuu wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda amesema
Takukuru ndiyo wenye kazi hiyo kwa sasa.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala amesema
Takukuru inatakiwa kuzifanyia kazi tuhuma hizo kwa sababu ni rushwa kama
yalivyo matukio mengine ya rushwa.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA