Serikali ya Tanzania na Uswisi zimesaini Mkataba utakaowawezesha
Makachero wa Tanzania kwenda nchini Uswisi na kufanya uchunguzi katika
mabenki ya huko ili kupata taarifa sahihi za walioficha mabilioni toka
Tanzania.
Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Dr Augustine Mahiga na Balozi wa Uswisi nchini Florence
Mattli.
Hata hii ni moja ya hatua muhimu ya Serikali awamu ya tano katika kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.
========================
HUKU
kukiwepo na dhana ya kuwa kuna Watanzania wanaotorosha fedha na
kuzificha katika mataifa mbalimbali ikiwemo Uswisi, hatua moja muhimu
imefanyika katika kukabili suala hilo, baada ya serikali ya nchi hizo
mbili, kusaini mkataba muhimu.
HabariLeo Jumapili imebaini kufikiwa kwa makubaliano ya ushirikiano
muhimu wa kisheria kwenye masuala ya jinai, unaolenga kuwajengea uwezo
makachero wa Tanzania, kuchunguza masuala mbalimbali ya kiuhalifu nchini
Uswisi.
Mkataba huo umeenda mbali zaidi, kwa kuweka wazi kuwa kuanzia sasa
makachero hao, wanaweza kuchunguza fedha za Watanzania zilizohifadhiwa
nchini Uswisi, tofauti na awali ambapo sheria za nchi hiyo zilikuwa
zinazuia.
Mkataba huo umesainiwa hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya miaka 50
ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi. Uswisi ni nchi inayosifiwa
kuwa na huduma bora za kibenki huku ikiwa na sheria kali zinazowalinda
wateja wake.
Mkataba wa makubaliano hayo, ambao umeleta mwanga katika kukabiliana na
usiri wa fedha hizo, ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga na Balozi wa Uswisi nchini,
Florence Mattli.
Akizungumza na gazeti katika mahojiano maalumu kuhusu mkataba huo,
Balozi Mahiga alisema kuwa katika kuendeleza ushirikiano mzuri baina ya
nchi hizo, Tanzania itanufaika na ruhusa hiyo ya kufuatilia akaunti za
fedha Uswisi.
Alisema kuwa kipengele hicho, kimekubaliwa kwenye makubaliano na kwa
sasa hakuna tena kikwazo kitakachoizuia Tanzania kuchunguza akaunti
hizo.
Alisema kuwa hatua hiyo inatokana na Serikali ya Uswisi pia kuridhishwa
na namna ambavyo Tanzania imekuwa ikipambana na vitendo vya rushwa na
ufisadi, kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake chini ya uongozi
wa Rais John Magufuli.
Alisema, Uswisi imekuwa ni rafiki mkubwa wa Tanzania tangu enzi na enzi huku ikiisaidia katika uboreshaji wa sekta mbalimbali.
“Kweli hiyo ni hatua nzuri kwa Tanzania hasa kwa kipindi hiki ambapo
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikikabiliana na rushwa na kila aina ya
ufisadi na kwa hiyo ruhusa hii itasaidia kulinda fedha zetu
kutoroshwa,” alisema Balozi Mahiga.
Akijibu swali ni lini serikali itakuwa tayari kupeleka makachero nchini
humo, kuchunguza madai ya kuwepo kwa Watanzania walioficha fedha kwenye
benki za nchini humo, Balozi Mahiga alisema; “Siwezi kusema ni lini
hatua hiyo inaweza kuanza kuchukuliwa kwa kuwa zipo mamlaka zinazohusika
na utekelezaji wake, ila ninachoweza kusema ni kuwa hatua iliyofikiwa
ni ya msingi kwetu kama nchi.”
Zitto apongeza Mkataba Akitoa maoni yake kuhusu makubaliano hayo, Mbunge
wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT – Wazalendo ), mmoja wa wabunge
ambaye amekuwa akilizungumzia suala la ufichwaji wa mabilioni ya fedha
nje ya nchi, aliliambia gazeti hili kuwa kipengele hicho kwenye mkataba
huo ni kizuri na kitasaidia kupatikana kwa fedha zilizofichwa katika
benki za Uswisi.
Alitumia nafasi hiyo kuipongeza serikali kwa uamuzi huo uliofikiwa na
kusema ni hatua ya kimafanikio, hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo
zinatokana na nguvu za wanyonge, ambapo pia zilipatikana kinyume na
sheria. Balozi Mattli, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na
Uswisi, umekuwa ukiimarika zaidi kila siku, na kuwa nchi hiyo itaendelea
kuisaidia Tanzania kwa hali na mali.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA