Historia yake;
Samuel John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 huko wilayani Urambo Mkoa
wa Tabora. Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 –
1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957 na kuendelea
na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle School”.
Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana
Tabora yaani “Tabora Boys” kidato cha I – IV na cha V – VI.
Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta alijiunga Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria (L LB) mwaka
1964 na kuhitimu mwaka 1971.
Sitta amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu mwaka 1966, wakati
yuko mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi UDSM, wanafunzi
waligoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
na kukatwa mishahara yao baada ya JKT. Hoja ya wanafunzi ilikuwa na
mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa
mishahara minono na marupurupu makubwa?
Baada ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu Julius Nyerere alikubali
kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya
mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. Miezi miwili baadaye akatangaza
Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi
hao.
Watukutu wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo (Wote sasa marehemu) na
wengine kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile walichokiita haki
zao, (haki za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu Mwalimu Nyerere kwa
maneno makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa
Mwalimu”.
Mwalimu Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa
kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao”. Miezi kumi
baadaye, baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia akaamua
kuwarudisha chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo; Sitta na wenzake 7
walitiliwa ngumu, hawakurejeshwa chuoni.
Busara za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu aliliwe zaidi na kuandikiwa
barua mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na. C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na
C3/Ss.13 ya 9/07/1967. Mwalimu alikubali kilio hicho na kuwaruhusu
vijana hao wanane warudi kwa sharti kwamba wale watukutu wawili (Sitta
na Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu Nyerere” mwenyewe. Hii
ndiyo ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM na kuendelea na masomo
kwa miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971.
Wakati Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya
Mafuta ya “CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 –
1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na
Mkurugenzi wa Utawala.
Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya
Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu
Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976.
Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta alikuwa kiongozi wa juu wa CCM na
serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na Waziri katika nyakati tofauti na
ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo wa vyama vingi.
Sitta alimuoa Margareth Simwanza Sitta
Mbio za ubunge
Enzi za chama kimoja 1975 - 1995 Sitta alikuwa mbunge wa Jimbo la Urambo
(kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia
alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi
cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.
Mwaka 1995 Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi
na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa
NCCR. Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda
kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta.
Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye uchaguzi
mkuu na aliwashinda wapinzani wake wakuu Lumatiliza Yotamu Lubungila wa
NCCR na Wilson George Ntakamulenga wa CUF. Sitta alipata kura 28,660
(72.3%) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki. Kurudi kwa
nguvu kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa
Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa aliloliita bunge la
"Speed and Standards" kwa mafanikio na changamoto nyingi.
Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda
wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (Chadema) na Zombwe
Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 (70.47%). Baada ya ushindi
huo, Sitta alijaribu tena kuwania uspika bila mafanikio; utendaji wake
wa kuiuma serikali na wakati mwingine kuipuliza kwenye Bunge la Tisa
ulimfanya achukiwe na serikali.
Ilipoonekana ana nguvu akatengenezewa “chui wa karatasi” (mshindani),
Andrew Chenge. Chenge naye akachukua fomu ya uspika ghafla,
likatengenezwa ‘zengwe’ kuwa wagombea wote wana nguvu, hapo CCM ikapata
mwanya wa kutamka kuwa haiwataki wote ili kuondoa mvutano. Sitta
akapoteza ndoto za uspika na ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda.
Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010 alimpa
Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kama Waziri,vilevile alihamishiwa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Mbio za urais
Samuel John Sitta alianza mbio za urais “kimyakimya” tangu alipokuwa
Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010). Kuna nyakati alikuwa akitoa kauli
zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti huku
akionyesha kuwa nchi ina viongozi thabiti na hawajapewa uongozi mkuu wa
nchi, akiwemo yeye.
Hata alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka 2014, mara nyingi Sitta
alionekana kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na alipohojiwa, mara
kwa mara, juu ya urais alionyesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa,
alilalamika kuwa wala rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi.
Katika Uchaguzi wa 2015, Sitta alitangaza nia ya kuwania Urais na
alichukua fomu ya kugombea urais kupita chama cha Mapinduzi ambapo baada
ya uchaguzi wa ndani chama, John Magufuli ndo jina lililofanikiwa
kupenya na kuteuliwa na chama kugombea Urais wa Tanzania.
Mungu Ailaze Roho Ya Marehemu Mahali Pema Peponi Amen.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA