Anna Mghwira: Tafakuri za mwisho wa mwaka 2016

Kipindi hiki cha sikukuu na mwaka mpya ni wakati wa matafakuri ya kila aina: Binafsi, familia, kazi na majukumu ya umma, kwa makundi mbalimbali na kwa umma wa nchi yetu, afrika na dunia kwa ujumla.


Nitatoa tafakuri langu kila siku ya kipindi hiki,kadiri itakavyowezekana. Huu utakuwa mchango wangu mwisho wa mwaka huu kwa kila msomaji.

Ninaomba tufuatane na tujadiliane pamoja kwa kila tafakuri. Asanteni Sana.

TAFAKURI LA KWANZA:

Msomaji mmoja ameniandikia akisema: Mama asante kwa salaam za Krismas ila mwaka huu tunakula makande tu kwa siku kuu, akiashiria ugumu wa maisha na kukatika ghafla mapato. Hili ni jambo la kweli na muhimu kujadili.

Tafakuri yangu inaniambia hivi:
Serikali imezuia mzunguko haramu wa fedha kwa kudhibiti mianya yake. Hili ni jambo jema likifanyika bila kuathiri maisha ya wananchi. Ili ubora wa udhibiti huu usiwadhuru wananchi walio wengi, wachumi waishauri serikali hatua za kuchukua ili mzunguko halali ufanye kazi. Watu wachache walifaidika na mzunguko haramu wa fedha. Tuwabane hao bila kuumiza umma usiohusika.

Ni kweli hali ya watu wasio na uhusiano na udhaifu wa kiuchumi ndio pia wanaathirika zaidi. Ili tusiangamie sote kwa kukosa maarifa; tutoe njia mbadala ya kupambana na uharibifu uliojitokeza ili kuokoa mamilioni wasiohusika.      

Chapisha Maoni

0 Maoni