Hashimu Rungwe kuibukiwa kwenye kesi ya Ndama Mtoto wa Ng'ombe


Wakili wa kujitegemea, Hashimu Rungwe amejitokeza kumtetea mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Ndama Shabani Hussein maarufu kama ‘Pedeshee Ndama mtoto wa Ng’ombe’. 

Rungwe aliyekuwa mgombea urais kupitia Chaumma katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alijitokeza jana na kujitambulisha mahakamani kuwa ndiye atamtetea mshitakiwa huyo. 

Ndama mtoto wa ng’ombe (44) anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kutakatisha fedha na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu. 

Baada ya kujitambulisha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa alisema kesi hiyo imepangwa kutajwa, upelelezi bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine. Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27,2016. 

Mshtakiwa huyo alipelekwa rumande kwa sababu miongoni mwa mashtaka yanayomkabili limo shtaka la kutakatisha fedha ambalo halina dhamana. 

Katika kesi hiyo, Ndama anadaiwa kuwa Februari 20,2014 jijini Dar es Salaam, alighushi kibali cha kusafirisha madini kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha kilo 207 za dhahabu yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kwenda Australia wakati akijua si kweli. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Machi 6, 2014 jijini Dar es Salaam alitengeneza kibali cha Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha dhahabu hiyo kutoka Congo inatarajiwa kusafirishwa kwenda Australia. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 katika jiji la Dar es Salaam alitakatisha fedha kwa kufanya muhamala wa dola za Marekani 540,390 kwa kuelekeza ziwekwe katika akaunti namba 9120000085152 iliyopo katika benki ya Stanbic yenye jina la Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited na kuanza kuzitoa taslimu wakati akijua fedha hizo zinatokana na zao la uhalifu.

Chapisha Maoni

0 Maoni