Maofisa waandamizi wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Tawi la Kariakoo, Dar es Salaam na mfanyakazi mmoja, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na makosa ya kujipatia Sh milioni 66 kwa njia ya rushwa.
Maofisa hao ni Liberatus Rugumisa (30), Keneth Mawere (29) na mfanyakazi mmoja Nassoro Nassoro (42) wote wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Lupyana Mwakatobe alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kwa madai ya kumpunguzia kodi mfanyabiashara Humphrey Lema kinyume na sheria zao.
Katika mashitaka ya kwanza, Mwakatobe alidai kuwa Novemba 18 mwaka huu, maeneo ya ofisi za TRA Kariakoo wilayani Ilala, Rugumisa na Mawere wakiwa waajiriwa wa mamlaka hiyo, walijipatia rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa Lema kwamba wangempunguzia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, alidai kuwa Novemba 23 mwaka huu, katika duka la kubadilishia fedha la Cate lililopo kati ya mtaa wa Nyamwezi na Donge, Kariakoo wilayani Ilala, walijipatia Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara huyo kwa madai watampunguzia VAT.
Katika mashitaka ya tatu ambayo yanawakabili washitakiwa wote, inadaiwa washitakiwa walijipatia rushwa ya dola za Marekani 2,744 sawa na Sh milioni sita kutoka kwa Lema kwamba wangeweza kumpunguzia VAT, kinyume na maadili ya kazi hiyo.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana. Hakimu Sachore alitaja masharti hayo kuwa ni wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika, watakaosaini bondi ya Sh milioni mbili. Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA