Rapa mkali katika anga ya Bongo Fleva anayetamba hivi sasa na ngoma yake ya 'Dume Suruali' amesema anayafurahia sana maisha ya ndoa tofauti na inavyodhaniwa na vijana wengi wenye uoga wa kuingia katika maisha hayo.
Mwana FA ambaye bado anaishi katika 'ndoa changa' akiwa amefunga mwezi Juni mwaka huu, amesema kabla ya kuingia kwenye maisha ya ndoa alisikia mengi ya kuogopesha, ambayo pia yanawatisha tamaa vijana wengine hususani wasanii na kujikuta wakiogopa lakini kwa upande wake anaona ndani ya ndoa kuna raha na furaha tofauti na maisha nje ya ndoa.
Mkali huyo wa ngoma ya 'Bado nipo nipo kwanza' aliyoitoa takriban miaka 7 iliyopita iliyokuwa ikitisha vijana kuoa, amesema aliyoyaimba katika ngoma ile ni ya kweli, na yalimsaidia kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kuingia kwenye ndoa na ndiyo maana ndoa yake haina mambo kama yale aliyoyaimba katika ngoma ile.
FA amefunguka hayo alipokuwa kwenye kipindi cha FNL cha EATV na kutoa ushauri kwa vijana wanaodhani kuwa ndoa ni ngumu kwa kusema "Ndoa siyo ngumu kama inavyofikiriwa na wengi, cha cha msingi muelewane, kila mtu ajue unachofanya, na kuheshimu nafasi yake ndani ya ndoa, maisha ya ndoa ni mzuri sana, tangu nimefunga ndoa, sioni tabu naona raha tu"
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA