Historia na simulizi: Nyerere Alipoingiwa Huruma Mwana-Tanu Mwenzake kukosa Nauli.

Leo Ni Tisa Disemba. Ni Siku yetu kuu kusheherekea Uhuru wetu. Tumetimiza miaka 55 ya uhuru. Tuna kila sababu za kusheherekea.


Nitapenda niweke hapa simulizi ya kihistoria yenye kusisimua, na kuelimisha pia.

Kwenye andiko lake lililojenga nadharia ya kisiasa. ' The Prince' kwa maana ya Mwana Mfalme, Mwanafalsafa Machiavelli anazungumzia juu ya kiongozi aweje. Machiavelli anamtaka kiongozi kuwa makini na tabaka la waliomsaidia kuingia madarakani na hata wenye kumzunguka. Kwa mujibu wa Machiavelli, hutokea kwa Mwana Mfalme "kuwajeruhi" waliomsaidia kuupata utawala.
Hii ni kwa kutowatimizia yote yale waliodhani kuwa ni haki yaokutimiziwa.

Badala yake, Mwana Mfalme huwaingiza kundini wawe kama wengine.
Katika manung'uniko yao, Mwana Mfalme hawezi kutumia dawa chungu dhidi
yao kwa vile hujihisi ana deni kwao. Lakini, cha msingi kwa MwanaMfamle ni kuzingatia ukweli, kuwa, hata kama atakuwa na maaduiwachache, katika kuchukua nchi, muhimu ni kuwaridhisha walio wengi, nahapa ni wananchi.

Huwezi kutawala kwa amani bila upendo na utashi wa walio wengi. Ni kwa sababu hizi, Mfalme Louis XII wa Ufaransa aliweza kwa kasi ya ajabu kuitwaa Milan na kwa kasi ya ajabu kuipoteza Milan.

Hakukidhi matakwa na matarajio ya wananchi walio wengi waliomfungulia
milango.Mtawala aliye mbali na asiyejali maslahi ya watu wake walio
wengi ni mtawala mwenye hofu. Na mtawala mwenye hofu zaidi na watu
wake kuliko adui wa nje, basi, hujijengea kasri ama ngome imara ya
kujihifadhi ingawa hilo halitamsaidia kuzuia nguvu za umma za
kumwondoa madarakani. Kwa mtawala, kasri ama ngome iliyo imara ni
kuepuka kuchukiwa na wananchi, kuacha ubinafsi na kujali maslahi ya
wengi.

Ni katika hili, kuna ambao walimtarajia Julius Nyerere kuwapendelea wale waliomsaidia kuingia kwenye mamlaka. Lakini, Nyerere aliwaacha waingie kwenye kundi kuu, kwa maana wawe miongoni mwa wananchi. Wafanye kazi ya siasa lakini si kwa kupewa vyeo vya juu, kwa vile tu, walikuwa ni miongoni mwa wale 17 waliounda TANU.
Hapa nawazungumzuia watu kama akina Chifu Kunambi na Dossa Aziz. Chifu Kunambi alitoa hata eneo lake kwa maekari ili kijengwe Chuo Kikuu. Chifu Kunambi amekufa miaka kadhaa iliyopita akiwa anaishi maisha ya kawaida pale Ubungo Msewe.

Na kuna , Julius Nyerere alimuonea huruma sana Dossa Aziz alipokutana nae kule Kizota , Dodoma. Dossa Aziz alikuwa ni MwanaTanu mwenye kadi nambari 4. Ni Dossa Aziz aliyetoa Landrover yake itumike na TANU, ndio gari aliyotumia Nyerere kuzunguka vijijini kwa wananchi kuitangaza TANU. Ni Dossa Aziz na wenzake waliomchangia Julius nauli ya kwenda UNO kudai uhuru wa Tanganyika.

Lakini, pale Kizota, Dodoma, miaka ile ya 80 mwishoni, Julius Nyerere alimwona Dossa Aziz aliyechoka sana. Julius akaambiwa, kuwa hata nauli ya kwenda Dodoma, Dossa Aziz alisaidiwa na rafiki yake na classmate wake wa tangu Kitchwele School, Ally Sykes.

Julius Nyerere aliingiwa na huruma. Inasemwa, kuwa Julius, kwa fedha zake mwenyewe, alimnunulia Dossa Aziz gari la kutembelea.

Chapisha Maoni

0 Maoni