Wadau kadhaa wa mpira wa miguu, wamemzawadia gari Jonesia Rukyaaa mwamuzi mwandamizi wa FIFA ambaye hivi karibuni alichezesha vema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake iliyofanyika nchini Cameroon.
Jonesia, ambaye amepata pia kuchezesha mchezo wa watani wa jadi katika soka nchini miaka miwili iliyopita, alichezesha mechi ya awali na kuonekana kutokuwa na upungufu kwenye kutafsiri sheria 17 za soka, alipangwa kuchezesha mechi ya mshindi wa tatu kati ya Ghana na Afrika Kusini.
Umahiri wake, umevutia wengi wakiwamo wadau wa mpira wa miguu ambao hawakupenda kutajwa walioamua kumzawadia gari aina Toyota Vits ikiwa ni zawadi na kumbukumbu yake baada ya kuiwakilisha vema nchi.Kwa upande wa TFF ilimtuza Mwamuzi Jonesia cheti cha kutambua uwezo na kufikia hatua ya kulitangaza shirikisho na nchi kwa ujumla. Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi ndiye aliyemkabidhi funguo za gari Jonasia.
Rais Malinzi alimsifu Jonesia kwa ujasiri na hatua aliyofikia na kumpa baraka za kumtakia mafanikio zaidi ya hapo ya kusonga mbele baada ya kufanya vema kwenye michuano ya Afrika Mashariki ya wanawake (CECAFA challange) na hiyo ya Wanawake Afrika.“Ni Mtihani mkubwa to officiate (kuchezesha) mechi kubwa kama hiyo. Maana kila kosa linaweza kukuondoa na mafanikio ya kupata medali ya dhahabu kati ya waamuzi wanne ni hatua kubwa inayopaswa kutuzwa. Siwasemi FIFA, lakini itoshe kusema kuwa Jonasia unaweza kufika hatua ya kuchezesha fainali za kombe la dunia,” alisema Malinzi.
Rais Malinzi alipigia upatu kwa waamuzi wanaume nao kuandaliwa vema na kuchezesha michezo mikubwa ikiwamo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwani kinachohitajika ni mikakati tu na kuitekeleza.“Kamati ya waamuzi nawaachia kazi hii. Maana kazi kubwa ya uamuzi ni kusoma na mazoezi,” alisema Malinzi mbele ya baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Waamuzi akiwamo Mwenyekiti wake, Saloum Chama.
Jonesia ambaye wakati wote alikuwa na faraja, alimshukuru Mungu kwa mafanikio aliyofikia pia wadau wote wakiwamo wazazi wake na bibi yake aliyemlea baada ya kufariki mama yake mzazi na viongozi mbalimbali ambao aliwaelezea kumtia moyo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA