Chama cha CUF kimeingizwa kwenye kile kinachoitwa mgogoro wa uongozi kwa
kisingizio kwamba eti Maalim Seif anataka kukiuza chama hicho kwa chama
cha CHADEMA. Profesa. Lipumba ni mtaalam wa uchumi na hesabu, na ndiyo
silaha kubwa katika kufanya uchambuzi wa masuala ya kiuchumi. Kwa mtu
kama mimi na wale tuliokwenda shule pamoja naye hapo chuo kiku cha Dar
es salaam hatuwezi kukubali hoja kama hizi kutolewa na mtu anaeitwa
Profesa wa uchumi.
Kwa kweli ni aibu. Sasa nimeelewa kwa nini yule babu wa Arusha aliweza
kuwahadaa watanganyika wote wakiwemo viongozi wakuu wa serikali, kwa
kusema amepata dawa ya kila maradhi kwa kuwanywesha maji ya mti wa
ajabu. Sasa si shangai vipi wananchi wenye u-albino wamekua wakiuliwa,
kwa baadhi ya wananchi kuamini kwamba wanaweza kupata utajiri, na mwisho
sasa sishangai vipi baadhi ya wananchi walikua wanakamatwa na kuchunwa
ngozi kwa kudhani tu kwamba ngozi hiyo ikifanyiwa matambiko unapata
utajiri.
Inasikitisha sana kwamba baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru bado hatuko
huru, hatuja zinduka na hatujaweza kujitambua na kujikomboa. Tujipime
kwa kujiangalia tulivyofanikiwa kwenye chaguzi huko nyuma, tuone kwamba
hoja hii ya kuuzwa chama cha CUF kwa chadema inasimama vipi.
1. Profesa akiwa ndiye Mgombea Urais wa chama cha CUF mwaka 2010,
alipata kura za urais 695,667 sawa na asilimia 8.28% na Dr. Slaa wa
Chadema alipata 2,271491 sawa na asilimia 27.05% . Mwaka huo hapakua na
ukawa na wala hakukuwa na ushirikiano wa vyama.
2. Mwaka 1995 na 2000, Chadema hawakuweka Mgombea urais na kura tulizopata CUF ni, 418,973 1995
na mwaka 2000 tukapata kura 1,329,077, sawa na 6.43% na 16.5%. Miaka 10
hiyo tulikosa hoja ya msingi ili kupata kisingizio cha kuwalaumu
wazanzibari au chadema. Muda wote kisingizio chetu ni dola ya CCM
kutofanya uchaguzi huru na wa haki.
3. Uchaguzi wa 2005 tukapata kura 1,327,125 sawa na 11.68 % takriban
sawa na zile za uchaguzi wa 2000. Katika uchaguzi wa 2010 tukafanya
vibaya sana na kura zetu kushuka hadi 695,667 takribani sawa na zile za
1995.
4. Baada ya miaka 20 kushiriki uchaguzi chini ya uongozi wa miaka 15 ya
Profesa. Lipumba na mara zote akiwa ni mgombea wetu wa urais tunapata
kura chache. Uchaguzi huo wa 2010, pia hatukupata hoja ya kuwasingizia
wazanzibari kukiuza chama kwa chadema.
5. Si mara moja wala mbili Profesa. amesikika akisema kwenye misikiti
kwamba kwa makusudi waliamua kumuachia Mhe. Kikwete ili ashinde eti kwa
sababu ni Muislam mwenziwawo wa Tanganyika. Mwisho wa mwezi wa Novemba
2016 Sheikh. Khalifa Khamis wa msikiti wa Mtoro amelalamika sana juu ya
uonevu unaofanyiwa wa-Islam na jinsi walivyokua wameendelea kukibeba
chama hicho (CCM) katika chaguzi zote. Alisema kwamba bila waislam wa
CCM , chama hicho mwaka 2015 kilikua ICU, yaani chumba cha wagonjwa
mahtuti. Kama si fyokofyoko za Lipumba si ajabu kingeondoka madarakani
mwaka huu 2015.
6. Badala ya kuuweka wazi ukweli huo, Profesa. anasingizia ukawa ndio
uliokikosesha ushindi chama cha CUF huku akijua kwamba yeye ndiye
muanzilishi wa Ukawa na jina hilo limeasisiwa na yeye binafsi kwenye
kikao cha umoja wa wabunge wa Bunge la Katiba hapo kwenye ukumbi wa
Msekwa Dodoma. Ni Profesa akiwa mwenyekiti wa ushirikiano huo aliyeweka
saini makubaliano ya pamoja juu ya kuweka mgombea mmoja wa Urais kwenye
uchaguzi wa 2015. Ulipofika wakati wa mgombea mmoja awe siye yeye ndipo
akaanza kusingizia nafsi kumsuta.
7. Katika hali ya kuonekana ni mwenye uchungu na hasira juu ya kuvurugwa
kwa Bunge la katiba alitoa hotuba ya kuwashawishi wabunge wa upinzani
wa bunge hilo kutoka kwenye bunge hilo kwa msingi kwamba tukishiriki,
tutakua tunahalalisha katiba ya CCM chini ya kivuli cha Bunge la katiba.
Hali ya mjadala wa bunge hilo ulivyotawaliwa na ubaguzi wa kidini na
kikanda na asili za watu Profesa. alichukia na kuwaita CCM ni wabaguzi
kama wale wa Ruwanda walioitwa Ntarahamwe. Hotuba zake hivi sasa ni
tafauti kabisa ya zile za Bunge la katiba. Kumbe wakati akisema yale
yeye mwenyewe ni mmoja ya CCM aliyevaa ngozi ya kondoo. Kutushawishi
kututoa ilikua ni agizo la CCM ili CCM wapate nafasi kufanya watakavyo
katika kupindua maoni ya wananchi ya Tume ya Mzee warioba. Hivyo yeye ni
ntarahamwe kupita CCM. Kwa nini sasa anafanya hivi nitaeleza baadae.
8. Hoja ya kuuzwa chama anayoitumia kukiuwa chama hiki (CUF) ni ya
kushangaza maana siku tulipokwenda kumuona nyumbani kwake kabla
hajajiuzulu, mimi na Maalim Seif, yeye alikua mbioni anakimbilia
kumfuata Mr. Mbatia ili kukamilisha mazungumzo ya kumleta Lowassa,
kwenye upinzani na ni yeye aliependekeza kwetu kwamba Mzee Lowassa
ajiunge na aidha NCCR au Chadema na kwamba CUF imuunge mkono. Sisi
tulikubaliana nae baada ya kutushawishi kwa takwimu alizotueleza kwamba
amepewa na wazee wa chadema kwamba akija Mzee Lowassa tutashinda kwa
asilimia 60 au zaidi.
9. Ni vizuri kujiuliza kwa kigezo gani cha msingi au cha kitaalam cha
Ukawa na au kuja kwa Lowassa alichonacho Profesa, kumlaumu Maalim kwamba
ndiye kisirani wa kutaka kukiuza chama cha CUF kwa Chadema?
10. Chama cha CUF 2010 kiliweka wagombea katika majimbo 132 huko bara,
ambayo yalikua na jumla ya kura 6,002,623. Katika majimbo hayo tulipata
kura za wabunge 639,402 sawa na 10.65% ya kura hizo.
11. Mwaka 2015, tumeweka wabunge katika majimbo 86 tu, 2, ya zamani na
50, tuliyopewa na Ukawa. Ziada ya majimbo 34 ni yale tuliyoweka wenyewe,
25 katika hayo tulipambana na CCM bila chadema wala NCCR. Jumla ya kura
za majimbo hayo 86 ni 4,398,666 , kati ya kura hizo, CUF tulizopata ni
1,112,246 sawa na 25.29%. Majimbo machache chini ya ushirikiano tumepata
kura nyingi, kuliko majimbo mengine tulipokua peke yetu chini ya
uongozi wa Profesa. Wingi huu wa kura kutoka 695,667 hadi 1,112,246
hakuwezi kabisa kutafsirika kwamba chama kimeuzwa , wingi huu
umetuongezea ruzuku kwa zaidi ya shs. 11 milioni kuliko ile ya 2010
tulipokua peke yetu.
12. Siamini na nitakua nahitaji kikombe cha babu wa Lolipndo, kwamba
kupata kura nyingi ni kukiuza chama. Hoja hii ni dhaifu maana kama chama
ni kukiuza basi pale alipotuacha Profesa katikati ya maandalizi ya
uchaguzi ilikua ni kukiuza chama au kukiuwa,? Na yeye akijua kwamba
anakiuwa, lakini pamoja na wazee kumbembeleza alituacha tufe.
13. Vipi chama kinasemwa kimeuzwa wakati chini ya ukawa tumeongeza
wabunge kutoka 2 Tanzania bara hadi 10, na kupata madiwani kutoka 152
tukiwa peke yetu hadi 285, tumepata Halmashauri 5, manaibu Meya 3,
ushindi ambao hatujawahi kuupata kwa maisha yote ya chaguzi
tulizoshiriki peke yetu chini ya uongozi wa Profesa.
14. Chini ya ukawa tumeshinda Urais wa Zanzibar, tumeongeza majimbo
kisiwa cha unguja kutoka 2, hadi 10 na kuiweka CCM kukataa kutoa
Serikali na hivyo kupindua ushindi wetu fawahisha.
15. Tungetegemea Profesa afurahie matunda haya hasa yale ya kushinda
uchaguzi huo huko Zanzibar. Cha ajabu badala ya kushiriki kupambana
tupewe serikali yetu ya CUF Zanziba yeye anapinga tusipewe na anakubali
kumtambua Dr. Muhammed Shein eti kumkomoa Maalim Seif .
16. Suala ni Je, kweli Profesa alikua mwanachama wa kweli kwa miaka yote
hii 16 ya uongozi wake au alikua ni pandikizi lililopewa kazi maalum
kuhakikisha kwamba CUF haishindi na wala haipewi Serikali? Tulishindwa
kumjua kwa sababu alikua hajapata majaribu katika uongozi wake. Pale
maslahi yake yalipopata mtihani akajidhihirisha mwenyewe kwa kuchukua
hasira za kujiuzulu, pamoja na kuombwa asifanye hivyo wakati huo wa
uchaguzi.
17. Hulka ya binaadam ni kwamba unapompa uongozi ndipo hujidhihirisha
alivyo, si kwamba hua amebadilika. Hivyo ndivyo alivyojidhihirisha
Profesa Lipumba kwamba kumbe hakua mwenzetu zamani sana.
18. Profesa alipotuachia chama wakati wa maandalizi ya uchaguzi aliamini
kabisa kwamba tutashindwa kusimama na hivyo kupata hoja ya kutusuta
pale tungeshindwa vibaya katika uchaguzi huo. Muungu alitulinda kwa
sababu nia zetu anazijua yeye.
19. Baada ya kuona chama hakikufa ndipo akatumwa tena kuja kukimaliza
kiwe hakipo kabisa. Maana suala la kujiuliza ni tangu lini Profesa awe
rafiki na Polisi. Tangu lini Profesa atumie uchochezi wa lugha za CCM
katika kugombanisha wafuasi wake wa CUF kwa kutegemea eti ndo anarudi
kukijenga? Utakujaje kujenga chama kwa kukigawa pande mbili. Kwa nini
utumie nguvu za dola ambayo ndiyo adui wetu mkubwa kutaka kurudi kwenye
uongozi wa chama ulioukataa mwenye? Wapi duniani penye mfano wa kiongozi
mnafiki kama huyu, kuacha uongozi kwa hiari yake na akaondoka kwenye
kiti chake hicho kwa mwaka mzima na hapo tena akazinduka kwamba anafuta
uamuzi huo. Haijapata kutokea labda uwe umekunywa kikombe cha babu wa
Loliondo.
20. Katika uachaji wake wa uongozi hivyo tulitakiwa tusubiri muda gani
mpaka tukubali kwamba sasa Profesa hayupo kwenye kiti chake hicho. Je,
tulikua tungojee miaka minne au mitatu au hadi mwaka mmoja kabla
uchaguzi mkuu wa 2020 ndipo tuamini kwamba sasa Profesa hayupo tena
kwenye kiti chake.
21. Ni aibu, na ndiyo maana nikasema tunahitaji kikombe cha babu, maana
ilivyotarajiwa hivi sasa tuwe tunaimarisha chama chetu kujiandaa kwa
uchaguzi wa serikali za mitaa. Badala yake leo CUF chama chenye nguvu,
tupo mahakamani tunagombanishwa wenyewe kwa wenyewe huku CCM imekaa
pembeni inachochea na kutucheka.
22. Katika hali hii watanganyika mujitambue kwamba munasafari ndefu sana
ya kujikomboa, maana akili zenu zimefinyangwa kwa miaka 50 kama unga wa
chapatti, hadi kuamini kwamba shida zenu ndiyo raha ya maisha yenu. Na
ufakhari wa kijana wa Tanganyika ni ubabe na matusi, kama vile walivyo
viongozi wa CCM na vijana wao. Badala ya kuona aibu kwa tabia hizo
Profesa mzima nae anaona hiyo ni sifa. Ninasema haya kwa ushahidi wa
Takwimu.
23. Nimepitia matokeo ya chaguzi za Jamhuri ya Muungano tangu hapo 1995
na kuangalia vipi vyama vya upinzani kwa jumla vilivyofanikiwa. Katika
kipindi chote hicho ushindi wa vyama vya upinzani wakiwa mmoja mmoja na
kwa pamoja hauja fikia asilimia 30 (30%) ya ushindi wa chama cha CCM.
24. Uchaguzi wa 2015 tulipojiunga vyama vine katika mazingira magumu ya
mfumo uliopo tumeweza kupata asilimi 40, (40%) ya kura za Rais ambazo ni
sawa na asilimi 68.3% ya kura za urais za CCM. Hii ni dalili njema. Pia
vyama viwili hivi vimeweza kupata asilimia 44. 5 (44.5%) ya viti vya
CCM.
25. Takwimu hizi zinatuambia kwamba kama lengo ni kuiondoa CCM
madarakani basi tukiungana pamoja wapinzani, CCM inaondoka 2020 , hata
kama itatumia nguvu za dola.
26. Hii ndiyo moja ya sababu kubwa za kutumiwa Profesa kuuwa CUF ili
kuuwa ukawa. Hivyo Profesa hakuja kujenga chama cha CUF ametumwa
kukamilisha kazi kabla 2020. Mialiko ya kuitwa Ikulu mara baada ya
uchaguzi na kesi zake kufutwa ghafla ni sehemu ya utamu wa kutiwa bei.
27. Hivyo asitafutwe mchawi na kupakana matope yasiyo mvua, Profesa
tangu awali alikuja CUF kama afisa mwenye kazi maalum, kutumung’unya
ndani kwa ndani kama dumuzi la gunia la mahindi, maana muda wote dalili
zikionesha kwa wepesi wake ndani ya chama.
28. Wakati ulipofika amejidhihirisha mwenyewe kwa kupoteza imani ya
wanachama. Imani ikishapotea hairudi. Hakuna tena atakaeamini kwamba
akiongoza CUF hatoacha tena kabla uchaguzi mkuu 2020. Profesa amerudi
kukimaliza chama siyo kukijenga. Asionewe Maalim Seif. CCM si mjinga wa
kumjenga Profesa kwa matumaini kwamba amuachie serikali ya CCM 2020.
Hizo ni ndoto za alinacha. Profesa akimaliza kazi ya kukiuwa CCM hawana
habari nae kama vile wasivyo na habari na wale waliotumika huko nyuma
ndani ya chama hiki.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA