Hoja sita za Mbunge Lema kusikilizwa leo

Hoja sita za mawakili wa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kupinga kunyimwa dhamana zinatarajiwa kusikilizwa leo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Salma Maghimbi.


 Wakili Sheck Mfinanga anayemwakilisha Lema alisema waliwasilisha hoja hizo za rufaa kupinga uamuzi wa kunyimwa dhamana mteja wao.

 Lema aliyekamatwa Novemba 2, akiwa mjini Dodoma, tangu wakati huo anashikiliwa kwenye Gereza Kuu la Kisongo jijini Arusha ambako amekaa kwa siku 56.

 Baada ya kukamatwa na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Lema alipewa dhamana na Hakimu Mkazi Desdery Kamugisha katika kesi namba 440 na 441/2016 akidaiwa kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

 Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama kumpa dhamana mbunge huyo.

Mawakali wa Lema nao walikata rufaa kupinga mteja wao kunyimwa dhamana ambayo imepangwa kusikilizwa leo baada ya kukwama kwa muda mrefu kutokana na kuwapo pingamizi za kisheria zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri.

Chapisha Maoni

0 Maoni