Ukiwa umetimia mwezi mmoja, baada ya Msaidizi wa Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benard Saanane (pichani) kupotea, Jeshi la Polisi limesema linachunguza taarifa za kupotea kwake ambazo ilizopokea kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama rafiki wa Saanane Desemba, 5, 2016.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari, Desemba 21, 2016 Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, CP Robert Boaz amesema Jeshi la polisi limefungua jalada la uchunguzi na kwamba taratibu za kiupelelezi za mtu aliyepotea zilifuatwa na bado upelelezi wa suala hilo unaendelea.
“Tuanashukuru wananchi wanaotupatia taarifa kuhusu tukio hilo, tunaahidi kwamba taarifa hizo tutazifanyia kazi. Tunazidi kuwaomba wananchi wenye taarifa za kupotea Saanane waziwasilishe katika kituo chochote cha polisi,” amesema.
Sambamba na hilo, Kamishna Boaz amefafanua tukio la uzikwaji wa maiti saba zilizokufa maji katika mto Ruvu, pasipo kufanyiwa uchunguzi wa kutambua waliokufa na chanzo cha vifo vyao.
“Mtakumbuka kati ya tarehe 6 hadi 12, 1016 huko mto Ruvu jeshi la polisi lilipata taarifa ya kuonekana maiti saba zikiwa zinaelea mtoni kwa nyakati na maeneo mbalimbali, baada ya taarifa hizo kupatikana askari na daktari walifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa kitaalamu,”amesema na kuongeza.
“Kutokana na ukweli kwamba baadhi ya maiti zilikuwa zimeharibika, maiti 6 ziliamuliwa kuzikwa katika eneo la tukio na moja yenye unafuu ilipelekwa hospitali ya wilaya ya Bagamoyo kwenye chumba cha maiti hadi pale ilipozikwa na halmashauri baada ya maiti hiyo kutotambuliwa na mtu yeyote.”
CP Boaz amesema hatua zote za kitaalam zilifuatwa na kwamba upelelezi unaendelea kufanywa ikiwemo wa kuwatambua marehemu hao na kujua chanzo cha vifo vyao
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA