Rais wa Gambia Yahya Jammeh amesema kuwa atakataa jaribio lolote la viongozi wa eneo la magharibi mwa Afrika la kumlazimisha kuondoka madarakani licha ya kushindwa katika uchaguzi na mpinzani wake, Adama Barrow.
Akihutubia Wanachama wa Muungano nchini humo Bw. Jammeh amesema: ”Waje wajaribu kuniondoa wanasubiri nini? mimi ni mtu mpenda amani lakini haimaanishi kwamba sitalitetea taifa langu, kwa ujasiri na uzalendo na kuibuka mshindi”.
“Mimi sio muasi, haki yangu haiwezi kuvurugwa. Hii ni nafasi yangu, hakuna mtu anayeweza kuniondoa labda Mungu,” amesema.
Amesema kuwa alikataa wito wa Muungano wa Viongozi wa Mataifa ya Magharibi ECOWAS akiwemo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria na Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia kuondoka nchini Gambia.
“’Wao ni kina nani wa kuniambia mimi niondoke nchini mwangu,” amesema na kuwashutumu viongozi hao kwa kuingilia mambo ya ndani ya Gambia.
ECOWAS tayari imesema kuwa inamtambua Bw. Barrow kama Rais wa taifa hilo na kwamba litachukua hatua zozote kuhakikisha kuwa matokeo ya uchaguzi yanaheshimiwa.
Viongozi wa eneo hilo watahudhuria kuapishwa kwa Bw. Barrow mnamo mwezi Januari 18 kulingana na taarifa ya Ecowas.
Rais Jammeh awali alikuwa amekubali matokeo ya uchaguzi huo mnamo Desemba 1, 2016 lakini baadaye akaitisha uchaguzi mpya utakaoandaliwa na tume ya uchaguzi inayomcha Mungu kwa madai kuwa matokeo hayo uchaguzi yaligubikwa na dosari.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA