Tangu juzi usiku habari hiyo ndiyo ilikuwa mjadala kwenye vyombo vya habari, mitandao na kijamii, ndani ya vyombo vya usafiri na vijiweni. Lakini kwa upande mwingine zilikuwa ni saa 48 nzito zilizoambatana na vikao mfululizo, kutenguliwa uteuzi na kuteuliwa kwa mkurugenzi mpya.
Alhamisi iliyopita, Dk Malecela alitoa tamko la kuwepo kwa ugonjwa huo.
“Sampuli za damu kutoka watu 533 zilipimwa. Kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya watu 533 waliopimwa, 83 sawa na asilimia 15.6 wamegundulika kuwa wameambukizwa virusi vya zika,” alisema Dk Malecela.
Siku iliyofuata, mtaalamu huyo wa tafiti za magonjwa yanayosambazwa na wadudu, akiambatana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliongea na waandishi wa habari kurekebisha taarifa yake, akisema alinukuliwa vibaya.
Suala hilo liliibua maswali kwa wadau, ambao baadhi wameitaka Serikali itayarishe utafiti mwingine ili ueleze ukweli kama ugonjwa huo upo nchini.
Pia, waliishauri Serikali kutoa elimu itakayowasaidia Watanzania kujua ugonjwa huo unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga badala ya kusubiri utafiti.
Zika ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya aedes anayeuma mchana na husababisha vipele, udhaifu wa misuli na kwa wajawazito husababisha wazae watoto wenye kichwa kidogo na ubongo mdogo.
Akizungumzia suala hilo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kufanyika kwa utafiti mwingine utakaoleta majibu halisi ya kuwapo au kutokuwapo kwa ugonjwa huo.
Alisema matokeo halisi ya utafiti huo yatasaidia kuiondolea jamii wasiwasi walioupata baada ya NIMR kutangaza utafiti wake na baadaye wakaukanusha.
“Nashauri zifanyike tafiti nyingine ili kuondoa wasiwasi kwa majibu yaliyokwishatangazwa. Hata kama yatakanusha, tayari vyombo vya habari vimeshayafikisha mbali na dunia inajua Tanzania kuna zika. Ni utafiti tu unaweza kusaidia kwa sasa,” alisema.
Sanga alisema mgongano uliojitokeza baina ya NIMR na Wizara ya Afya, unatokana na pande hizo mbili kutoshirikishana katika hatua za utafiti, hadi matokeo yalipotangazwa.
“Kila taaluma inayo maadili yake, likiwamo suala la utafiti, kKwenye suala zito kama hili ambalo dunia inalitazama, ingependeza kama kungekuwa na umakini zaidi, ili kuondoa mkanganyiko uliojitokeza hivi,” alisema.
Kuhusu hatua zilizochukuliwa na Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Dk Malecela, Sanga alisema kwa kuwa tatizo ni namna taarifa zilivyotangazwa bila wizara husika kujua na si utafiti, ni sawa kuwajibishwa wakati majibu sahihi yakitafutwa.
Mtafiti na mtaalamu wa masuala ya kilimo, Dk Aloyce Kulaya alisema suala la utafiti ni la kitaalamu na kisomi na yeyote anayefanya utafiti anapaswa kujiridhisha kabla ya kuamua kuutangaza.
Hata hivyo, alisema baada ya kazi ya utafiti kufanywa na kutangazwa, haipaswi mtu yeyote kuibuka na kuupinga iwe kisiasa au kwa njia nyingine yoyote na badala yake utafiti hupingwa kwa utafiti mwingine.
“Ninavyoelewa mimi, haipaswi kwa mtu au taasisi kufanya utafiti wake mara moja, utafiti unapaswa kurudia zaidi ya mara moja ndipo uweke hadharani na mtu anapokuwa hakubaliani nao anapaswa kuujibu kwa utafiti,” alisema Dk Kikuya.
Alisema ni vyema kwa watafiti wanapofanya kazi zao, hususan zile zinazohusu masuala muhimu na yanayoigusa jamii, kuwa makini na kujiridhisha kabla ya kutoa matokeo hadharani.
Mtafiti mwingine aliyebobea kwenye masuala ya kisaikolojia, Frank John pia alisema ni wakati ambao Serikali inapaswa kufanya utafiti mwingine na kutoa majibu yatakayomaliza malumbano yaliyopo.
Akizungumzia nafasi ya wasomi katika kuishauri Serikali, Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo alisema kusimamishwa kazi kwa Dk Malecela ni pigo kwa uhuru wa wanataaluma na wasomi.
“Je, Serikali itafungia pia journal (jarida) iliyochapisha utafiti huu? Ni pigo kiasi gani kwa taaluma na uhuru wa wasomi?” alihoji Profesa Kitila katika akaunti yake ya mtandao wa Twitter.
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Profesa Kitila alikiri kuandika hivyo na kusisitiza kuwa Serikali ilipaswa kushauriana na NIMR kuliko kumwondoa Dk Malecela.
“Haiwezekani kulifuta lile chapisho. Matokeo yake yameshachapishwa, hayawezekani kufutwa, labda kama kuna kasoro za kitaaluma. Andiko hilo linaonyesha lilishawasilishwa kwenye mkutano wa wanasayansi likakubalika, kwa hiyo wananchi wanaweza kulipitia wakitaka,” alisema Profesa Kitila.
Alisema Wizara ya Afya ilitakiwa kukutana na uongozi wa NIMR ili kushauriana, kuliko hatua hiyo.
“Walichofanya Wizara ya Afya si sahihi kwa sababu Dk Malecela ameeleza matokeo ya utafiti, wangewasiliana na uongozi wa NIMR.
“Kuna utafiti uliotolewa na Benki ya Dunia ulioonyesha kuwa nusu ya wafanyakazi wa sekta ya afya hawana uwezo wa kutibu wagonjwa, ulitolewa bila kumshirikisha Waziri wa Afya. Mbona hawakulalamika?” alihoji na kuongeza:
“Hata sheria za utumishi bado hazijavunjwa kwa sababu Dk Malecela alikuwa anawasilisha matokeo ya utafiti siyo taarifa ya ugonjwa.”
Taaluma imedhalilishwa
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema uamuzi wa kumtimua Dk Malecela umeidhalilisha taalama nyeti ya afya nchini.
Dk Mashinji ambaye ni mtaalamu wa afya ya binadamu, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa katika ziara ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema katika Kanda ya Nyasa kukagua uhai wa chama na kufanya uchaguzi wa kanda.
Dk Mashinji alitoa wito kwa wataalamu wote nchini kuungana kupinga vitendo vinavyokiuka na kukandamiza ustawi wa taifa, huku akiwataka kutotoa ushirikiano kwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya.
WHO yanena
Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) limesema halina taarifa za kuwepo dalili wala mgonjwa wa zika Tanzania.
Mwakilishi wa shirika hilo, Dk Grace Saguti alikuwa akijibu swali kama shirika hilo hupata taarifa za magonjwa mbalimbali ya mlipuko kutoka Wizara ya Afya.
“WHO inafanya kazi na Wizara ya Afya kufuatilia taarifa za magonjwa kila siku katika maeneo yote ya afya, na taarifa huletwa wizarani kisha tunashirikishwa ili kutoa katika tovuti yetu. Ninachoweza kusema hatujapata taarifa za magonjwa ambazo zinazoonyesha dalili za mgonjwa yoyote mwenye zika Tanzania,” alisema Dk Saguti.
Mganga Mkuu wa Serikali, Mohamed Kambi alisema Wizara ya Afya ina mfumo wa kupata taarifa kuhusu magonjwa na kupitia mfumo huo hazijapatikana taarifa za kuwapo wa mgonjwa wa zika.
Kambi aliwasihi wanataaluma, watafiti na wanasayansi wakitaka kutoa taarifa zozote kujihakikishia usahihi wa taarifa hizo kabla ya kuzitoa.
Imeandikwa na Elias Msuya, Tumaini Msowoya, Geofrey Nyang’oro, Muyonga Jumanne na Joyce Mmasi wa Mwananchi
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA