Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi akiambatana Mkurugenzi wa manispaa na vyombo vya ulinzi na usalama leo ametembelea ghafla ofisi za kampuni ya mawasiliano ya Zantel iliyoko katika eneo la Msasani.
Katika ziara hiyo Mh. Hapi amebainisha kuwepo kwa mkataba uliokuwa umefichwa baina ya manispaa ya Kinondoni na kampuni ya Zantel wa kuweka mitambo yake katika eneo la wazi la Msasani linalomilikiwa na manispaa ya Kinondoni.
Licha ya kuingia mkataba huo mwaka 2009, Hapi alidai kuwa nakala ya mkataba huo ilinyofolewa katika kumbukumbu za manispaa hiyo, na pia kampuni ya Zantel haijawahi kulipa kwa manispaa ya Kinondoni kiasi cha dola 45,000 (zaidi ya milioni 90) kwa mwaka kwa miaka 8 tangu mwaka 2009.
Akizungumza na uongozi wa kampuni hiyo Hapi ameagiza kulipwa kwa fedha hizo zote pamoja na malimbikizo ya thamani tangu mkataba huo uliposainiwa. Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni bwana Aron Kagurumjuli amemkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Zantel hati ya madai ya malipo (invoice) na kuagiza fedha hizo zilipwe ndani ya siku saba vinginevyo manispaa ya Kinondoni itaanza kutoza riba.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni ameagiza vyombo vya dola kuanza uchunguzi mara moja kujua ni kwanini mkataba huo ulinyofolewa katika kumbukumbu za manispaa ya Kinondoni na kama kuna mtu aliyehusika na ufisadi huo akamatwe mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
"Hapa kuna harufu ya ufisadi. Vyombo vya dola Takukuru na Polisi, nataka muanze uchunguzi mara moja kubaini wahusika wote waliohujumu serikali kwa miaka yote hii na kuikosesha mapato haya." Alisema Hapi.
Katika hatua nyingine DC Hapi ameagiza manispaa ya Kinondoni kuweka utaratibu wa kuzitumia fedha zitakazolipwa katika ujenzi wa madarasa ili wanafunzi wanaokosa fursa ya kusoma wapate elimu.
"Kwa fedha hizi tunaweza kujenga zaidi ya madarasa 40. Ambayo ni sawa na shule mpya tatu zenye madarasa 12 kila moja na ofisi. Naagiza Mkurugenzi simamia zilipwe na ziende katika elimu." Alisema DC.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ametoa rai kwa makampuni yote ambayo yanashiriki kuhujumu mapato ya manispaa yajisalimishe mara moja, kwani muda wao unahesabika.
"Tutapitia mkataba mmoja baada ya mwingine, hata ile iliyonyofolewa kwenye mafaili. Yeyote anayejua ana mapato ya serikali na hajalipa ajisalimishe au ajiandae kukutana na nguvu ya dola. Lakini njia hii ya pili itakua na maumivu yake.."
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Zantel alimueleza Mkuu wa Wilaya kuwa amepokea maagizo hayo na kwamba atayafikisha kwa Mkurugenzi Mtendaji ambaye yuko Zanzibar kikazi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA