Kijana wa UVCCM Arusha aliyejifanya Usalama wa Taifa asomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM, Mkoa wa Arusha (UVCCM), Lengai ole Sabaya, amesomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili ya kujifanya mtumishi wa umma katika Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Akisomewa maelezo hayo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Gwantwa Mwankuga, wakili wa serikali, Riziki Mahanyu, alidai katika kesi hiyo upande wa serikali unatarajia kuwa na mashahidi watatu na vielelezo vitatu.

Aliwataja mashahidi hao kuwa ni Meneja wa Hoteli ya Sky Way, Filipo Siake, Ofisa Usalama wa Taifa Mkoa wa Arusha, Editha Aveline na Mpelelezi wa Kituo cha Polisi Arusha, Rogathe huku akitaja vielelezo watakavyowasilisha kuwa ni kitambulisho cha TISS ambacho kina jina na picha ya Sabaya, risiti ya Hoteli ya Sky Way yenye namba 0983 pamoja na hati ya kuchukua mali.

Akimsomea hoja hizo za awali, Wakili Mahanyu alidai kuwa Mei 18 mwaka huu, Sabaya alifika katika Hoteli ya Sky Way na kuchukua chumba ambacho alitakiwa kulipa Sh 30,000 kila siku ambapo alikaa hotelini hapo kwa siku tano.

Wakati mshitakiwa anaingia hotelini hapo alikabidhi mali zake ambapo ni Ipad aina ya Samsung Galaxy na kitambulisho cha usalama wa taifa alichosema ni cha kwake.


Chapisha Maoni

0 Maoni