Majambazi yavamia mgodi, yaua wawili na kujeruhi wanne huko Bahi

WATU wawili wamekufa huku wengine wanne wakijeruhiwa baada ya majambazi walio na silaha kuvamia mgodi wa dhahabu wa Nholi uliopo wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Majambazi hao wanadaiwa kupora dhahabu, fedha na mali nyingine na kuwavua watu nguo na kuondoka nazo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe alikiri kupokelewa kwa miili ya watu wawili hospitalini hapo na majeruhi wanne.
Alisema mwili mmoja upo katika hali mbaya. Waliofariki dunia katika tukio hilo, walitajwa kuwa ni Lukumale Membo na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Hamisi.
Kwa mujibu wa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Melisiana Danford, maiti hao na majeruhi walipokelewa hospitalini hapo saa 6 usiku kuamkia jana mara tu baada ya kutokea kwa tukio hilo. Majeruhi katika tukio hilo ni Sunday Undi (49), Lawrence Mhagama (35) , Maila Mchele (44) na Sophia Sayuni (37).
Wakizungumza katika wodi namba moja ambako wamelazwa, majeruhi hao walisema walivamiwa na majambazi, ambao baadaye waliwapiga risasi na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine kujeruhiwa.
Lawrence Mhagama ambaye amepigwa risasi mguu wa kushoto, alisema amekuwa akiendesha shughuli za uchimbaji mdogo kwenye mgodi huo. Alisema siku ya tukio majira ya saa mbili usiku akiwa ndani, alisikia milio ya risasi nje na alipojaribu kutoka, alipigwa risasi ambayo ilimjeruhi mguuni.
“Chanzo cha tukio kwa kweli sikijui ila majambazi walituvamia , mimi ni mgeni eneo hilo nilikwenda kwa ajili ya kazi ya mgodi, nimepigwa risasi mguuni ambapo mpaka sasa bado ninayo mwilini, wanasema wataniruhusu nikipata nafuu na baadaye wataangalia uwezekano wa kuitoa risasi hiyo,” alisema.
Alisema majambazi hao, walipora mali nyingi ambapo waliwavua watu nguo na kuondoka nazo huku wakiacha watu uchi.


Majeruhi mwingine aliyelazwa wodi namba moja, Sunday Undi, alisema walivamiwa na majambazi hao majira ya saa mbili kasorobo usiku wa kuamkia juzi, wakiwa kwenye kioski cha Maila Mchele, wakipata vinywaji na kuendelea na mazungumzo.


“Tulivamiwa tukasikia tunaambiwa tuko chini ya ulinzi, kwa vile lilikuwa ni tukio la kushtukiza tukawa tunashangaa, wakapiga risasi juu ikabidi tuingie ndani ya kibanda kile baada ya muda tukajikuta watu saba tukiwa chini ya kitanda,” alisema.


Alisema majambazi hao waliwaamrisha watoke na kuwaambia kila mtu atoe alichonacho na aliyekuwa akikataa, aliamriwa kuvua nguo.


“Walininyang’anya fedha na simu, wakatuvua na suruali wakaondoka nazo, mimi binafsi wamenipora Shilingi milioni mbili nilizokuwa nazo,” alisema.


Alisema majambazi hao walikuwa zaidi ya wanne na walikuwa wamevalia kininja. Alisema mtu aliyejaribu kuwatazama usoni, alikuwa akipigwa risasi. Majeruhi mwingine katika tukio hilo, Maila Mchele ambaye amelazwa wodi hiyo akiwa hajitambui, amejeruhiwa vibaya.


Inadaiwa alipigwa risasi tumboni na kutokea upande wa pili. Majeruhi wa nne, Sophia Sayuni (37) amelazwa wodi namba 10 hospitalini hapo.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alisema atalitolea ufafanuzi baadaye.


Chanzo-Habarileo

Chapisha Maoni

0 Maoni