WAKATI vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) vikitarajiwa kuanza kuketi ndani ya saa 24 zijazo jijini
Dar es Salaam, joto la mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama hicho
limepanda na kufikia kiwango cha juu.
Kuwapo kwa mabadiliko hayo kunachagizwa na uamuzi wa hivi karibuni
kabisa wa Rais Dk. John Magufuli kuwateua watu wenye nafasi nyeti za
uongozi ndani ya chama hicho kushika nafasi mbalimbali za kiserikali.
Uamuzi wake wa kuwateua Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi,
Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Pindi Chana na kabla ya hapo Dk. Asha Rose
Migiro ambao wote ni wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho kuwa mabalozi,
inatajwa kuwa msingi na chachu ya kutokea kwa mabadiliko.
Aidha, hatua ya kumteua Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kunatajwa pia kuwa hatua nyingine inayochagiza
kuingia kwa sura mpya katika nafasi nyingine kadhaa ndani ya vikao vya
sekretarieti na kamati kuu vya chama hicho.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya CCM, zinaeleza
kuwa, baada ya kamati kuu kumaliza kikao chake cha siku mbili
keshokutwa, uko uwezekano wa kutokea kwa mabadiliko makubwa yanatarajiwa
kutangazwa Jumanne katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC).
Miongoni mwa mabadiliko yanayotarajiwa kutokea ni yale yatakayogusa
nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara) iliyokuwa
ikishikiliwa na Luhwavi.
Mbali ya hilo, upo uwezekano wa Mwenyekiti Magufuli kutumia fursa hiyo
kuwateua watu wapya kuongoza idara za chama hicho ambazo wakuu wake
wamepewa majukumu mapya ya kiserikali.
Miongoni mwa idara hizo ni ile ya mambo ya nje iliyokuwa ikiongozwa na
Dk. Migiro na ile uenezi na itikadi ambayo kwa muda mrefu imekuwa
ikiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye.
Baadhi ya makada wa muda mrefu wa CCM wamelieleza gazeti hili kwamba,
hatua ya Rais kuwateua Luhwavi, Nchimbi, Pindi Chana na kabla ya hapo
Dk. Migiro katika nafasi za ubalozi, upo uwezekano mkubwa kwa wateule
hao wapya kutangaza kujiuzulu nafasi zao za ujumbe wa CC ndani ya chama
hicho tawala.
Iwapo hilo litatokea, mambo mawili yanaweza yakaandamana na uamuzi wao
huo, la kwanza likiwa ni kwa Mwenyekiti Magufuli kujaza nafasi zao na wa
pili ukiwa ni kuondoka kwa wajumbe wengine wote wa Kamati Kuu kama
ilivyopata kutokea miaka minne iliyopita.
Wajumbe wanaounda Kamati Kuu ya CCM kwa sasa ni Rais wa Zanzibar, Dk.
Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula.
Wengine ni Katibu Mkuu wa CCM,Abdulrahman Kinana.
Wamo pia, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Spika wa Baraza la Wawakilishi.
Wengine ni Luhwavi, Vuai Ali Vuai, Nnauye, Muhammed Seif Khatibu, Zakhia
Meghji, Asha Rose Migiro, Sophia Simba, Sadifa Juma Khamis, Abdallah
Bulembo.
Wengine ni Jenister Mhagama, William Lukuvi, Steven Wasira, Nchimbi,
Chana, Jerry Slaa, Adam Kimbisa, Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Mwinyi na
Maua Daftari.
Wapo pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Dk. Salim Ahmed Salim, Makame Mbarawa na Hadija Abood.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuingia katika Kamati Kuu ni lile la
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye anapewa nafasi kubwa
ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi.
Mbali na hayo, nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho inayoshikiliwa na Kinana ndiyo inayoonekana kupandisha zaidi joto hilo.
Taarifa kutoka ndani ya CCM zinadai kuwa, ni mapema kusema iwapo Kinana
ambaye katika miaka ya hivi karibuni amekuwa nguzo muhimu ya utendani
anaweza kuondolewa katika nafasi hiyo, kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa
ndani unaokikabili chama hicho mwakani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, upo uwezekano mkubwa wa Kinana kuendelea
kubaki katika nafasi hiyo pamoja na Makamu Mwenyekiti CCM- Bara, Phillip
Mangula, mwanasiasa anayetajwa kuwa karibu zaidi kiimani machoni mwa
Dk. Magufuli.
Viongozi hao wawili wakongwe katika chama hicho, wanapewa nafasi kubwa
ya kuendelea na nyadhifa zao ili kuweza kukiongoza chama hicho kuelekea
katika mabadiliko kamili makubwa mwakani.
Hata hivyo, wakati Kinana akipewa nafasi ya kuendelea kushikilia wadhifa
huo, taarifa nyingine zinamtaja mwanasiasa kijana, Mwigulu Nchemba kuwa
mtu anayeweza kubebeshwa mikoba ya ukatibu mkuu wa CCM.
Mwigulu, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliwahi
kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho wakati Rais Mstaafu Dk. Jakaya
Kikwete alipokuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya CCM kililieleza gazeti hili kuwa
mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli, anayo nafasi kubwa ya kutumia
vikao hivyo kuunda Kamati Kuu mpya ambayo itazaa sekretarieti mpya ya
chama hicho.
Kuwapo kwa hisia za kufanyika kwa mabadiliko katika kamati kuu na kwa
wakuu wa idara wanaounda sekretarieti kumeonekana kuwavuruga baadhi ya
wana-CCM ambao wanaonekana kuyahofia mabadiliko hayo.
“Hapa ndipo joto linapoanzia, si unajua mwenyekiti alivyo msiri, watu
hawaelewi kama viongozi wa sasa wataendelea au watawekwa pembeni,”
alisema mtoa habari mmoja.
Katika hatua nyingine, duru zaidi kutoka ndani ya CCM zinadai kwamba,
joto hilo la mabadiliko limeibua kundi la moja la watu wenye ushawishi
kuhofia hatua zozote ambazo zinaweza kumuondoa Katibu Mkuu, Kinana.
Kundi hilo linadaiwa kujenga ushawishi wa kutaka Kinana aendelee na
wadhifa alionao au nafasi yake ishikwe na mtu mwingine mwenye kukifahamu
vyema chama hicho.
Kundi hilo linadaiwa kumtaja Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi kuwa mtu pekee wanayemuona kuwa na uwezo wa kuvaa
viatu vya Kinana.
Julai 23, mwaka huu, wakati Rais Magufuli alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa CCM Taifa, alimuomba Kinana na sekretarieti nzima ya chama hicho
kuendelea kukitumikia hadi hapo yatakapofanyika mabadiliko mengine.
Ingawa hakusema atafanya lini mabadiliko ya sekretarieti yake, lakini
Rais Magufuli aliwashtua wale waliokuwa wana ndoto ya kumrithi Kinana
kwa kuwaambia kuwa “wamenoa”.
Vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC)
ambavyo vitafanyika hivi karibuni vitakuwa ni vikao vya kwanza tangu
Rais Magufuli achaguliwe kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Kufanyika kwa kikao cha NEC jijini Dar es Salaam na si Dodoma kama
ilivyozoeleka, kumeelezwa na baadhi ya wana-CCM kuwa kunatoa ishara ya
kufanyika kwa jambo kubwa ndani ya chama hicho.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA