Matukio: Polisi wakamata silaha za kivita mkoani Mwanza, wawili wauawa.


MWANZA ni hatari. Ndivyo alivyosema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, baada ya matukio mawili yaliyotokea usiku wa kuamkia jana, likiwamo la nyumba moja kukutwa silaha za kivita, za jadi na watoto 10 waliokuwa wakifundishwa mafunzo yanayoashiria kuwa ni ya kigaidi.

Silaha zilizokutwa katika nyumba hiyo iliyopo Bugaka, Kata ya Kishili jijini Mwanza, ni bunduki aina ya AK 47, mabomu ya kurusha kwa mkono, bunduki aina ya Maker 4, risasi zaidi ya 150, majambia na visu.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili katika mahojiano maalumu, Kamanda Msangi alisema kuwa aliongoza vijana wake kufika katika nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya watuhumiwa wanaowashikilia kwa matukio mbalimbali, kwamba wafadhili wao wapo Kishili na Buhongwa.

Msangi alisema kutokana na taarifa hizo, aliunda vikosi viwili kufanya operesheni maalumu usiku wa kuamkia jana, kimoja kilikwenda eneo la msitu wa Deo uliopo Buhongwa na kingine Kishili.

Akizungumzia kikosi cha Kishili alichokiongoza, alisema walipofika katika nyumba hiyo waliizingira na watu waliokuwamo ndani wakaanza purukushani za kutaka kujihami ndipo askari walilazimika kufyatua risasi moja kuwatuliza.

Kamanda Msangi alisema wakati wanatafuta namna ya kuingia ndani ya nyumba hiyo iliyo na uzio, kijana mmoja alifanikiwa kuruka ukuta kwa upande wa nyuma na kutoroka, lakini wakafanikiwa kuwadhibiti wenzake zaidi ya 15.

“Baada ya kuwadhibiti na kuingia ndani, tulifanya ukaguzi na kufanikiwa kupata mabomu ya kurusha kwa mkono yaliyokuwa yameandaliwa kwa matumizi, bunduki za kivita aina ya AK 47, magazine tano na kila moja ikiwa na risasi 30, majambia, bunduki ndogo aina ya Maker 4, visu na gari moja ambayo inawezekana ndiyo wanayotumia kufanya doria zao kabla ya kufanya matukio.

“Tulipoingia tumewakuta watoto wadogo 10 waliokuwa wakifundishwa mafunzo maalumu ya namna ya kutumia silaha walizokuwa nazo na namna ya kujilinda na adui, pia kulikuwa na wanaume wanne wakubwa na wanawake wawili ambao inaelezwa ndio watoaji mafunzo kwa watoto hao.

“Katika mahojiano ya awali, tumeelezwa kwamba watu hao wana vikosi katika mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, ikiwamo Tabora, Mwanza na Kigoma,” alisema.

Kamanda Msangi alisema wakati wanapambana na watuhumiwa hao, wananchi walijikusanya eneo hilo, wakiwa na nia ya kutaka kuwaua watuhumiwa hao, lakini askari walisimama imara na kufanikiwa kuondoka nao wakiwa hai.

Alisema baada ya kuondoka na watuhumiwa hao, baadaye alipata taarifa kwamba wananchi waliamua kuteketeza nyumba hiyo kwa moto alfajiri ya jana.

WAWILI WAUAWA

Akizungumzia kikosi cha pili kilichokwenda msitu wa Deo, alisema kiliambatana na vijana wanne ambao baadhi yao ni waendesha bodaboda, waliokuwa wakishikiliwa kwa matukio ya hivi karibuni.

Alisema walipofika katika msitu huo, walionyesha silaha zilipo na katika ukaguzi walifanikiwa kupata bunduki moja aina ya SMG, magazine mbili huku moja ikiwa na risasi 15 na nyingine 30, pia walikamata bastola moja.

“Wakati askari hao wakifanya upekuzi katika msitu huo, ghafla watuhumiwa hao walianza purukushani ya kutaka kutoroka, ndipo askari waliwafyatulia risasi na kuwaua wawili.

“Tunaendelea kuwahoji watuhumiwa ili kupata mtandao wote, lakini hapa Mwanza ni hatari, kibaya zaidi vijana hawa wa bodaboda wanajihusisha na vitendo hivi, tunaomba wananchi kuwa makini na kundi hili,” alisema.

Chapisha Maoni

0 Maoni