Ya CUF na Prof Lipumba: Prof. Lipumba azomewa na wananchi wa mkoa wa Lindi


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Prof. Ibrahim Lipumba amekutana na wakati mgumu baada ya wananchi wilayani Ruangwa mkoani Lindi kumzomea.

Prof. Lipumba alikumbana na hali hiyo alipokuwa mkoani humo katika ziara aliyoeleza kuwa ni ya kujenga chama. Akiwa anapita katika barabara huku gari lake likilindwa na vyombo vya ulinzi, wananchi waliokuwa wamesimama kando kando ya barabara walisikika wakiimba wimbo “Hatumtaki”, huku wengine wakimuita msaliti.

Mbali na wananchi hao waliokuwa wakimzomea, wengine walikuwa na mabango yaliyokuwa yakisomeka “CUF kwanza Lipumba baadaye”, “Hatukutaki msaliti wewe.”

Wakati hayo yote yakiendelea, Prof. Lipumba na viongozi wanaomuunga mkoani walikuwa ndani ya gari na hawakusema jambo lolote.

Kwa muda sasa kumekuwa na mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho kuhusu nafasi ya Mwenyekiti ambapo baadhi wanamtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti halali huku wengine wakumtambua Julius Mtatiro kuwa ndiye mwenyekiti halali.

Licha ya Prof. Lipumba yeye kuendelea kufanya mikutano ya ndani huku akipata ulinzi wa vyombo vya dola, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif alizuiwa kufanya mkutano wa ndani uliokuwa umepangwa kufanyika mkoani Mtwara.

Chapisha Maoni

0 Maoni