Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Ole Sendeka aanza ziara ya utambulisho kwa kutembelea halmashauri ya mji wa Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher ole Sendeka akisalimiana na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Njombe Dkt Samwel Ndalio Thomas mara baada ya kuwasili Halmashauri hapo. Kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha manunuzi na mweka hazina wa Halmashauri.
Mhe. Ole sendeka akisalimiana na Karani wa Fedha “Cashier” wa Halmashauri Neema Kalundwa 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri zilizofanyika.
Mhe. Ole sendeka akionesha nakala ya kitabu cha Ilani ya uchaguzi ambapo amewataka watumishi kuisoma na kila mmoja kuwajibika kwenye eneo lake la utekelezaji kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama Cha Mapinduzi.Kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Jackson Saitabahu akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Ruth Msafiri.

Hyasinta Kissima –Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka amekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa huo.

Akiwasilisha salamu za shukrani kwa mapokezi mazuri aliyopatiwa toka alipowasili Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa, Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa Mikoa ambayo alipendelea sana kufanya kazi kutokana na uwepo wa fursa nzuri za maendeleo, mandhari nzuri na hali nzuri ya hewa.

”Nimefurahi sana kuwa katika Mkoa huu kwani kwa kipindi chote nilitamani sana kufanya kazi katika MKoa wa Njombe na nilitamani sana kama nafasi hii niliyoipata ningeipata kipindi nilipokua kijana lakini bado nafuraha kubwa kwani ndoto yangu ya kuitumikia na kuifanya Njombe ya maendeleo imeanza kutimia kupitia uteuzi wa Mhe. Rais na ninawahakikishia kuwapatia ushirikiano wa kutosha katika yale yote mtakayoona yanahitaji uwepo wangu.”alisema Mhe.Ole Sendeka.

Awali akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri mbele ya Mkuu wa Mkoa Mkurugenzi wa Halmashauri Illuminatha Mwenda amesema kuwa, Halmashauri imejitahidi kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, ujenzi wa nyumba za waalimu katika shule mbalimbali za sekondari, utoaji wa mikopo ya vijana na wanawake ambapo katika robo ya kwanza jumla ya Tsh. milioni 52 zilitolewa kutoka mapato ya ndani huku shughuli za ukusanyaji mapato mpaka kufikia sasa halmashauri imefikia asilimia 40% ya ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za ukusanyaji mapato(POS) 97 zilizopo katika maeneo yote ya ukusanyaji ushuru wa Halmashauri.

Mara baada ya kuipokea taarifa hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kwa sasa Chama Kilichopo Madarakani ni Chama Cha Mapinduzi chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, na hivyo watumishi wote hawana budi kuhakikisha kuwa wanaipitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kuhakikisha kuwa kila mtu anasoma katika eneo lake na atambue kwamba ni kwa namna gani anahusika katika utekelezaji wa ilani hiyo. 


Ameendelea kusema hatakuwa na huruma kwa watendaji watakaoshindwa kukiri mapungufu na kukubali kusahihishwa katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo na yeye hatakuwa na matatizo na mtumishi ambaye atatekeleza majukumu yake ipasavyo na amewaonya wanasiasa wanaochochea migogoro na kukwamisha shughuli za maendeleo kwani yeye hatakua na mswalia mtume kwa chama cha aina yeyote ile.

“Mkurugenzi Mhe. Rais amekuamini na amekuteua kuisimamia Halmashauri hii hakikisha kuwa unasimamia watendaji wako wote mpaka wale watendaji wa ngazi za chini Kabisa kama watendaji wa Vijiji, usiwaonee huruma kwani ukiwaonea huruma wale wa juu hawatakuonea huruma wewe na mimi pia sitakuonea huruma. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Halmashauri za Mkoa wetu zinakuwa za mfano kwa kuwa na watendaji wenye weledi na wachapakazi kama kauli ya Mhe. Rais inavyosema Hapa kazi tu.”ameendelea kusema

“Naipongeza Halmashauri kupitia taarifa yako Mkurugenzi kwa kuhakikisha kuwa kwa vipindi vyote Halmashauri ya Mji Njombe haijawahi kupata mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na msibweteke kwa kulewa sifa hizo bali hakikisheni Mji unaendelea kuwa msafi.

Mhe. Sendeka ameiagiza Halmashauri kuhakikisha kuwa inatenga maeneo ya upandaji miti kwa kadri halmashauri itakavyoshirikiana na wakala wa barabara (TANROAD ) na idara ya misitu na mazingira ili kuhakikisha kuwa wanapata aina nzuri ya miti itakayopandwa pembezoni mwa barabara za watembea kwa miguu, maeneo ya taasisi na kila mwananchi ahamasishwe kupanda mti nje ya eneo lake la makazi.


Awali kabla ya kukutana na watumishi wa Halmashauri ya Mji Njombe Mkuu huyo wa Mkoa alipata nafasi ya kutembelea mradi wa maji uliopo Kambarage na Ujenzi wa standi mpya ya Mabasi mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na amemtaka Mwandisi wa Ujenzi kumfikishia taarifa mapema hii leo ya sababu zilizopelekea mkandarasi wa mradi huo kuongezewa muda wa umaliziaji wa awamu ya pili ya ujenzi wa stand hiyo kinyume na mkataba.

Chapisha Maoni

0 Maoni