JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lililazimika kuingilia kati zoezi la uchaguzi wa Shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa CCM tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kunusuru hali ya amani na usalama,
Uchaguzi huo uliofanyika jana kuanzia majira ya saa tano asubuhi ukiwa chini ya usimamizi wa Enosi Lupimo, Katibu wa Shirikisho la vyuo vikuu CCM Mkoa wa Dar ulikuwa na lengo la kujaza nafasi zote za tawi hilo zilizo wazi baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza kipindi chao ulimalizika saa kumi na mbili jioni.
Sintofahamu iliibuka katika ukumbi wa uchaguzi mara baada ya zoezi la kupigia kura wagombea wa nafasi mbalimbali kuanza, ambapo baadhi ya wajumbe walihoji uhalali wa wapiga kura waliopo ukumbini kwani hawakuwa wamekaguliwa kama ni wanachama halali au la.
Hata hivyo Lupimo aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo alimtaka Daud Ngassa Katibu wa CCM tawi la UDSM aliyemaliza muda wake kutoa maelezo juu ya suala hilo. Ngassa alisema, “Hatujaja na reja ya wanachama wetu hapa lakini sijaona sura ngeni ukumbini, wote ni wanachama wa CCM.”
Baada ya maelezo hayo Lupimo aliwahoji wanachama ikiwa wapo tayari kuendelea na uchaguzi bila ya kukaguliwa majina na kadi zao katika daftari la wanachama au uchaguzi huo uhairishwe mpaka daftari lenye orodha ya wanachama litakapopatikana. Wanachama wengi waliridhia uchaguzi kufanyika huku wachache tu wakipinga.
Wagombea katika nafasi ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Umoja wa Wanawake (UWT), katibu mwenezi na nafasi ya katibu wa tawi walijinadi na kupigiwa kura huku nafasi ya mwenyekiti wa tawi ikifanywa ya mwisho kwa wagombea kujinadi na kupigiwa kura.
Katika matokeo ya nafasi hizo, ambapo Cristopher Masebo aliibuka mshindi katika nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi kwa kupata kura 92 dhidi ya kura 41 za Petro John.
Katika nafasi ya katibu wa tawi Onesmo Allan aliibuka mshindi kwa kupata kura 116 dhidi ya Abdallah Mkulo aliyepata kura 22.
Wagombea katika nafasi ya mwenyekiti wa CCM tawi la UDSM, Abiyani walikuwa ni Juliana Julius, Adelitus Mushumbusi na Mramba Abdallah.
Mgogoro mkubwa uliibuka ukumbini baada ya wagombea wote watatu wa nafasi hiyo kumaliza kujinadi na kuanza kwa zoezi la kupiga kura ambapo baadhi ya wanachama walidai kuwa karatasi za kupigia kura hazitoshi na kwamba baadhi ya watu walikosa.
Mvutano huo ulichukua muda kidogo kabla ya msimamizi wa uchaguzi kuamuru utaratibu wa kupiga kura ubadilike na wajumbe waliopo ukumbini wahesabiwe upya ili kubaini ‘mamluki’ waliodaiwa kujipenyeza ukumbini.
Baada ya wanachama hao kuhesabiwa ilibainika kuwa ni 91 tu waliokuwa ukumbini ilihali zoezi la upigaji kura lililofanyika hapo awali lilishindwa kuendelea baada ya karatasi 150 za kupigia kura kudaiwa kuwa ni chache.
Zoezi la upigaji kura liliendelea huku wanachama 91 tu wakiwa wamebainika kuwapo ukumbini. Hata hivyo baada ya kura kupigwa na zoezi la kuhesabu kura za nafasi hiyo kuanza jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 116, ikiwa ni ongezeko la kura 25 tofauti na wanachama halali waliokuwepo ukumbini wakati wa kupiga kura.
Suala hili lilizua mvutano mkubwa sana huku mvutano huo ukichukua muda pasipo maridhiano kupatikana, baadhi wakitaka matokeo hayo yatangazwe, wengine wakitaka uchaguzi uhairishwe na kundi lingine likitaka umakini uongezeke na zoezi la kupiga kura lirudiwe kwa wakati ule ule.
Kwa wakati huo matokeo ya kura zilizohesabiwa ambazo hazikuwa halalizl zilionesha kuwa Abdallah Mramba alipata kura 64, Adelitus Mushumbusi kura 44 na Juliana Julias kura 04 huku kura zilizoharibika zikiwa ni 04.
Wanachama wengi waliokuwepo ukumbini hawakukubaliana na matokeo hayo, wakihoji kura 25 zilizozidi zilitoka wapi? Swali ambalo halikuwa na mtu wa kulijibu na badala yake mvutano ukizidi kuwa mkali.
Msimamizi wa uchaguzi huo aliamua kuondoka ukumbini kwa muda wa dakika takribani 20 akifanya mawasiliano ya Jeshi la Polisi ili lifike katika eneo la uchaguzi kuimarisha ulinzi ili matokeo yaweze kutangazwa.
Ilikuwa ni Saa 10:43 jioni, ambapo askari wa Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa na gari aina ya Ashok Leyland yenye namba za usajili PT 3927 waliwasili katika ukumbi wa DDC Mlimani Park- eneo la uchaguzi.
Askari hao walihoji kinachoendelea, ambapo Lupimo aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi alieleza kuwa wanaomba ulinzi ili matokeo ya uchaguzi huo yatangazwe, hata hivyo Erick Bernard mmoja kati ya wanachama wa CCM alitoa maelezo kuwa wanapinga kutangazwa kwa matokeo hayo kwani kura zimezidi idadi ya wanachama halali waliopiga kura, na kutaka kurudiwa kwa zoezi la kupiga kura.
Said Said, mwenyekiti wa tawi hilo anayemaliza muda wake, alipinga hoja ya kutaka kurudiwa kwa zoezi la kupiga kura akidai kuwa wanachama wengi wameshaondoka ukumbini hivyo zoezi la kupiga kura haliwezi kurudiwa na wanachama waliopo. Kundi la wanachama lililokuwepo ukumbini lilitaka uchaguzi urudiwe kwa wakati huo kwa hoja kuwa waliopo ukumbini ndiyo wana CCM halisi na walioondoka ni mamluki.
Baada hoja hizo kinzani, polisi waliwasihi wanachama wabakie ukumbini huku wakiwachukua viongozi waliomaliza muda wao na wagombea wa nafasi ya uenyekiti na kwenda nao faragha ili kutafuta suluhu zaidi ya jambo hilo.
Iliwachukua takribani dakika 55 kabla ya kukubaliana kutangazwa kwa matokeo ya nafasi zote za uongozi isipokuwa nafasi ya mwenyekiti wa tawi iliyokuwa ikigombewa na Mushumbusi, Mramba na Bi. Juliana.
“Nafasi ya mwenyekiti wa tawi, uchaguzi utarudiwa katika tarehe itakayotangazwa upya na viongozi wenu na wagombea watakuwa ni walewale,” alitangaza Lupimo, msimamizi wa uchaguzi huo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA