KAMPUNI ya Kupakua na Kusafirisha mizigo ya ABG African Link iliyopo Buguruni Sukita, Dar es Salaam imeamriwa kuhama katika eneo walilopewa na Kampuni ya Jitegemee Trading Company inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kushindwa kulipa kodi ya pango ya Sh bilioni 1.3.
Aidha, Kampuni ya Udalali ya Yono, jana ilianza kutoa vitu mbalimbali vilivyokuwepo kwenye majengo ya kampuni hiyo baada ya notisi ya saa 24 waliyopewa kumalizika.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo ya udalali, Stanley Kevela aliliambia gazeti hili jana kuwa walitoa notisi kuitaka kampuni hiyo kuhama eneo hilo tangu Jumanne ambayo iliisha juzi.
Alisema Yono itaendelea kufuatilia deni hilo la kodi hadi litakapolipwa vinginevyo, itafuatilia mali na kuzikamata kwa ajili ya kuzipiga mnada.
“Watu wameona mali za chama kuwa ni sehemu ya kujineemesha, nasi kama kampuni tuna uchungu na chama, hivyo tutahakikisha fedha hizo zinapatikana na tutatafuta mtu anayestahili atakayewekeza katika eneo hilo,” alisema Kevela.
Akielezea tukio hilo, Meneja Uendeshaji wa kampuni ya ABG, Mmad Abubakar alisema si kweli kwamba wanadaiwa kodi hiyo, bali ni mgogoro wa kisheria kati yao na Jitegemee ambao waliingia mkataba tangu 2008.
Alisema walipewa eneo hilo la Sukita wakati huo likiwa shamba na lengo ni kuliendeleza na kwamba walipewa mkataba wa kukaa bure kwa miaka mitatu.
“Baada ya kupewa shamba tuliwaambia wabadilishe hati iwe ya biashara ambapo ilikuwa na namba 1010 iliyopatikana 2012 ndipo tukaanza ujenzi na muda wa kukaa bure umeisha 2015 ambapo tulikabidhiwa eneo lenye urefu wa meta za mraba 50,000,’’ alisema.
Alifafanua mwaka 2014, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliwapa barua kuuondoa ukuta uliokuwa pembezoni mwa mto Msimbazi na kujenga meta 60 kuingia ndani, hivyo kubakiwa na eneo la meta za mraba 12,000 kati ya meta za mraba 50,000 na kwamba kinachogombaniwa ni nani atagharamia ujenzi wa ukuta huo.
“Mkataba unatutaka uwekezaji usizidi dola 800,000 (Sh bilioni 1.7) ambazo tukihamisha ukuta huu gharama zitazidi. Tuliamua kukaaana Jitegemee, lakini hatukufanikiwa, tukaona ni vyema kufungua kesi mahakamani,’’ aliongeza Abubakar.
Kwa mujibu wa meneja huyo, kesi hiyo namba 84/2014 ipo Mahakama Kuu mbele ya Jaji Rose Temba kwa ajili ya usuluhishi, lakini wanashangazwa na kitendo cha kutolewa vitu vyao nje na kudai wanaiachia mahakama itende haki.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA