Hatua ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP), kuwafutia mashitaka ya ujangili watu tisa, wakiwamo
wenye nasaba na Mbunge wa Mbarali, Haroon Mulla; imeibua ‘kilio’
miongoni mwa watu walio katika mapambano dhidi ya ujangili nchini.
Kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao kunaelezwa kuwa ni jaribio kubwa kwa
uongozi wa Rais John Magufuli, ambaye ameapa kupambana na vitendo vya
ujangili ili kulinda wanyamapori.
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, ililazimika kufuta kesi
dhidi ya watu hao waliokutwa na bunduki 17 baada ya upande wa mashitaka
kuwasilisha maombi ya kufutwa kwa kesi hiyo.
Kwa uamuzi huo, watuhumiwa wote waliachiwa huru na kukabidhiwa bunduki
zao ambazo awali zilidaiwa kutumika kwenye mauaji ya wanyamapori, wakiwamo tembo 86.
Waliofutiwa mashitaka ni Mikidadi Mwazembe (55), Shahgol Mulla (42), Pirmohamed Mulla (25) na Fahad Pirmohamed (31).
Wengine ni Sylvester Lugolo (28), Mazar Gamdust (50), Abdulsamad Abdala
(22), Shahdad Mulla (42) na Juma Msagati (23). Wote ni wakazi wa Mbarali
mkoani Mbeya.
Hivi karibuni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Pirmohamed Mulla
alikamatwa na nyara za Serikali zikiwamo pembe za tembo na kupandishwa
kizimbani.
Alitiwa hatiani na kuhukumiwa kwenda jela miaka 20 au kulipa faini ya Sh
milioni 138.390. Mshitakiwa huyo alilipa kiasi hicho cha fedha na
kuachiwa huru. Katika mashitaka mengine, jangili Pirmohamed Mulla na
wenzake wanane, walifunguliwa mashitaka mengine ya uhujumu uchumi,
lakini Ofisi ya DPP kwa kushirikiana na Polisi, wakaamua kufuta
mashitaka hayo.
Habari kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na kikosi
kazi kilichoundwa kupambana na ujangili, zinasema hatua hiyo imewavunja
moyo watu waliojitoa uhai wao kuwalinda wanyamapori.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani.
Upande wa mashitaka ambao ni Jamhuri uliamua kuondoa mashitaka dhidi ya
washitakiwa wote.
Awali, washitakiwa hao walisomewa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mkoa wa Mbeya, wakituhumiwa kuua wanyamapori bila kuwa na vibali
halali vya Serikali.
Katika uamuzi wa Mahakama Kuu, Jaji Dk. Adam Mambi aliwaachia huru,
akisema kesi yao isingeendelea kwa kuwa upande wa mashitaka uliamua
kuondoa shauri hilo mahakamani.
Alisema washitakiwa hao katika kesi yao iliyokuwa Mahakama ya Hakimu
Mkazi ya Mkoa, walikuwa wakishitakiwa kwa tuhuma za uhujumu uchumi, na
kwamba wameachiwa kwa kutekeleza matakwa ya kifungu 91 cha Mwenendo wa
Makosa ya Jinai.
“Upande wa mashitaka ambao ni Jamhuri, ulifuta mashitaka yao katika
Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, hivyo kutokana na kufutwa huko, Mahakama Kuu
hatuwezi kuendelea kusikiliza mashitaka yaliyofutwa, hivyo na sisi
tunayafuta kwa mujibu wa sheria,” alisema jaji huyo.
Mashitaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, yalifutwa
na Hakimu Atughanile Ngwala baada ya upande wa mashitaka kuamua kufuta
mashitaka.
Katika kesi hiyo namba 6/2016 iliyofunguliwa Novemba 10, mwaka huu,
washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na kesi mbili za uhujumu uchumi
kupitia uwindaji haramu wa wanyamapori.
Waendesha Mashitaka wa Serikali – Basil Namkambe na Hebel Kihaka –
waliieleza Mahakama kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda kosa la
kuwinda na kuua wanyamapori waliokatazwa.
Kihaka aliiambia Mahakama kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo kwa
nyakati tofauti kati ya Agosti 2006 na Septemba 2014 katika mikoa ya
Mbeya, Tanga, Morogoro na Iringa ambako wanadaiwa kuwinda na kuua tembo
86 na wanyama wengine.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, aliwataka
washitakiwa wote kurudishwa rumande hadi Novemba 17 kesi itakapoanza
kusikilizwa.
Novemba 17, mwaka huu kesi hiyo iliitwa tena mahakamani hapo na ndipo
ilipofutwa kwa kile kilichoelezwa kuwa upande wa Jamhuri uliomba
iondolewe kutokana na upelelezi wake kutokamilika na kwamba ungechukua
muda mrefu.
Pia wanafamilia hao wanadaiwa kukutwa na bunduki 17 zinazosadikika
kutumika katika matukio mbalimbali ya ujangili katika Hifadhi za Taifa.
Bunduki hizo zilikamatwa katika makazi ya wanaukoo wa Mulla.
Mapya yaibuka
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii waliozungumza na
JAMHURI kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema mtuhumiwa mmoja kati
ya hao anamiliki bunduki saba.
“Bunduki kadhaa walizokutwa nazo zipo zilizonunuliwa madukani, lakini
kuna nyingine zimetoka katika vituo vya polisi nchini,” anasema mtoa
taarifa wetu.
Hadi sasa mtu mmoja aliyesaidia kikosi kazi kupata taarifa za ujangili
za watuhumiwa hao hajulikani aliko, akidaiwa kutekwa na watu
wasiojulikana.
“Huyu mtu ndiye aliyewezesha kukamatwa kwa hawa watuhumiwa, ametoa
ushirikiano ikiwa ni pamoja na kueleza idadi ya wanyama waliouawa kwani
naye alikuwa akihusika. Alikisaidia kikosi kazi, akiwa njiani kwenda Dar
es Salaam ametoweka na hajulikani alipo. Ingawa zipo taarifa kwamba
ndugu yake mmoja amehusika katika njama za kumpoteza,” anasema mtoa
taarifa.
Maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi walio kazini na wengine waliostaafu,
wanadaiwa kuwa kwenye mpango madhubuti uliofanikisha kuachiwa huru kwa
watuhumiwa hao.
Mmoja wa wasiri wa JAMHURI amesema kitendo cha kuwaachia watuhumiwa hao
wa ujangili, ni mkakati wa kukwamisha juhudi za kupambana na ujangili
ambazo zimeanza kuonesha mafanikio.
Amesema haiwezekani kesi za aina hiyo zifutwe katika mazingira
yasiyoeleweka kwa kisingizio cha kutokamilika kwa ushahidi, huku
watuhumiwa wakiwa wamekamatwa na ushahidi ukionesha wazi kuhusika kwao.
“Rais awe mkali, la sivyo atajikuta hawezi kupambana katika vita hii.
Mtandao huu ni mkubwa unaohitaji mapambano ya kweli kwani watu wa aina
hii wana pesa na wapo tayari kwa lolote,” anasema mtoa taarifa wetu.
Taarifa za uhakika ambazo JAMHURI imezipata zinaonesha kuwa kuachiwa kwa
watuhumiwa wa ujangili ni matokeo ya kufanikiwa kwa mtandao mkubwa
unaowahusisha baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi,
maofisa katika ofisi ya DPP, wanasiasa na watu mbalimbali wenye
ushawishi.
Mmoja wa watu wanaotajwa ni aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya (RPC) ambaye alihamishiwa katika moja ya miji mikubwa nchini, na
kwa sasa amestaafu.
“Huyu anajua mtandao wa ujangili unavyofanya kazi. Alikuwa karibu na
majangili wengi, na hata alipoondoka Mbeya alihakikisha anarithisha
uhusiano huo kwa waliompokea ofisi.
“Majangili wakikamatwa wanampigia simu, na yeye anatumia nafasi yake
kama mmoja wa wastaafu kuzungumza na ‘vijana’ wake kuweka mambo sawa.
Kufutwa kwa kesi nyingi za ujangili na dawa za kulevya ni matokeo ya
mtandao huo kuanzia Polisi Makao Mkuu, Ofisi ya DPP na hata kwenye ngazi
ya wale walio na nguvu au ushawishi kwenye kikosi kazi,” kimesema
chanzo chetu.
JAMHURI imepewa majina ya maofisa hao wanaotajwa kushirikiana na majangili, na kwa sasa inaendelea kuhifadhi majina hayo.
JAMHURI imewasiliana na Mwanasheria Ofisi ya DPP, aliyekuwa katika
kikosi kazi mkoani Mbeya, Paul Kadushe, ili kuweza kupata ufafanuzi
kuhusu kufutwa kwa kesi hiyo.
Amethibitisha kuwa ni kweli kesi imefutwa, lakini mwenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni Mwanasheria wa Mkoa.
“Mimi nilikuwapo awamu wa kwanza alipokamatwa Pirmohamed ambaye ni mtoto
wa mbunge, tukamfungulia mashitaka, Mahakama ikamuamuru kwenda jela au
kulipa faini ya Sh milioni 138 akalipa na kuachiwa huru.
“Baada ya hapo nilipangiwa majukumu mengine, nilienda mkoani Arusha
kwenye kesi ya Lema, hivyo kesi hiyo nyingine ilikuwa na wanasheria wa
mkoa. Ila nimesikia kuwa imefutwa, siwezi ongea zaidi ya hapo, Mbeya
wanaweza kukusaidia nini kilitokea mpaka ikawa hivyo,” amesema Kadushe.
Mwakilishi wa Ofisi ya DPP Mkoa wa Mbeya, Joseph Pamde, ameulizwa juu ya
kufutwa kwa kesi hiyo, lakini akaruka kwa madai kwamba si msemaji.
“Ofisi yetu ina taratibu, na taratibu ni kwamba anayepaswa kuongelea
mambo ya kesi mahakamani ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP); ukimpata yeye
atakwambia kila kitu kuhusu hiyo kesi unayoiulizia,” anasema Pamde.
DPP Biswaro Mganga hakupata kutokana na maelezo kwamba yuko nje ya nchi. Anatarajiwa kurejea nchini leo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA