RAIS
mstaafu wa Awamu ya Nne na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Jakaya Kikwete amewapoza wahitimu wa fani ya ualimu akisema wasikatishwe
tamaa na tatizo la ajira katika sekta hiyo kwa kuwa ni suala la muda
litakalokwisha muda mfupi ujao.
Dk Kikwete aliyasema hayo jana alipokuwa akiwajibu wahitimu wa Chuo
Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa waliopaza sauti wakimtaka amuombe Rais
John Magufuli afungue milango ya ajira katika sekta hiyo na sekta
nyingine za umma.
Mmoja wa wahitimu hao (jina lake halikupatikana) alisema, “Inaumiza
kuona wenzetu waliomaliza chuo hiki mwaka mmoja uliopita wakiendelea
kusota mitaani na sasa tunaungana nao katika msoto huo.”
“Ujumbe umefika,” Dk Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya
nane ya chuo hicho yaliyofanyika jana katika viwanja vya chuo hicho
mjini Iringa, alisema.
Aliwaambia wahitimu 952 aliowatunuku vyeti vyao katika fani nne za
Shahada za Elimu kwamba tatizo la uchelewaji wa ajira kwao litakwisha
baada ya muda mfupi kwa kuzingatia kwamba Taifa lina mahitaji makubwa ya
walimu.
Kikwete aliyetumia dakika zisizozidi tatu kuzungumza na wahitimu hao
wakati akifunga mahafali hayo, alisema ataufikisha ujumbe huo
kunakohusika kama alivyoombwa.
Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho Mkuu wa chuo hicho, Profesa
Bernadeta Killian alisema uongozi wa chuo unaendelea na mikakati
mbalimbali ya kukiboresha ili kiendelee kuwa taasisi na mahali bora pa
kutolea elimu, huduma za jamii kama vile ushauri na kuongeza udahili wa
wanafunzi.
Alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, chuo kimezalisha wahitimu 5,018 kama walimu katika fani mbalimbali.
“Aidha, idadi ya wanataaluma wenye shahada za uzamivu imeongezeka kutoka 0 mwaka 2006 hadi 26 mwaka huu,” alisema.
Pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, Profesa Killian alisema chuo
kinaendelea kuikumbusha serikali kuwa ruzuku inayotolewa kwa ajili ya
uendeshaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali bado ni ndogo na imekuwa
ikishuka mwaka hadi mwaka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya MUCE na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala alisema MUCE wana changamoto ya
uhaba wa walimu kiasi cha chuo kutumia wahadhiri kutoka vyuo vingine
kwa gharama ya ziada.
Pia upungufu wa wafanyakazi waendeshaji na upungufu mkubwa wa ofisi za
wanataaluma hali inayopelekea mazingira ya utendaji wa kazi kwao kuwa
mgumu.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Profesa Mukandala alisema chuo
kimechukua hatua kadhaa zilizo ndani ya uwezo wake, lakini ili
kuzimaliza inahitaji msukumo kutoka serikalini.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA