Uhakiki: Askofu Mokiwa ataka uhakiki wa madhehebu

Serikali imetakiwa kufanya ukaguzi kwenye taasisi za dini kwa sababu baadhi zinatoa mahubiri kinyume na Mungu.


Hayo yamesemwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa.

Amesema mahubiri yanayotolewa na viongozi wa taasisi hizo ni tofauti na mienendo na uhusiano wao na haziendani na wanayohubiri.

Ameongeza kuwa baadhi zipo kibiashara zaidi, siyo kwa ajili ya kuwasaidia waumini wake.

Dk Mokiwa ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kushiriki ibada ya kipaimara iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Filipo lililopo Ukonga Relini, Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam.

Pia, ameshauri ukaguzi huo ulenge taasisi zinazotumia majina ya watu, kwani Serikali imekuwa ikizisajili bila kuzifanyia tathmini kujua zinavyojiendesha.

“Serikali imekuwa na wakaguzi wa fedha. Basi utaratibu huu uwekwe hadi katika taasisi za kiimani. Serikali inaandikisha zaidi kuliko kukagua hivyo nawakumbusha,” amesema Dk Mokiwa.

Dk Mokiwa ametumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kujitayarisha kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka salama, siyo kusherehekea kuumaliza.

“Wajitayarishe kuwa na mabadiliko ya maisha mapya. Wale walevi waache, wenye kupanga nyumba sasa wajenge zao, wezi waache na watu wafanye kazi kwa bidii,” amesema.

Amewakumbusha vijana waliopata kipaimara kujihadhari na imani mpya.

“Hivi karibuni nilipita kanisa moja jipya, nikaona wamevaa nguo rangi nyekundu na wengine wamevaa magunia huku wakicheza ngoma,” amesema Dk Mokiwa na kuongeza:

“Lazima tuwakumbushe imani hizi ambazo zingine siyo salama, zikaguliwe misingi na mafundisho yake maana zinaganga njaa.”

Padri wa Kanisa hilo, Jackson Muhunda amewahimiza waumini wa dini mbalimbali kumrudia Mungu na kuachana na watu wanaojiita manabii na wanaodai wana miujiza ya kuwasaidia.

Chapisha Maoni

0 Maoni