Taarifa zilizotufikia hivi punde ni kwamba askari na maafisa mbalimbali
wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama hapa Nchini wanasikitika sana kuona
ahadi wanazopewa na viongozi wa Serikali zikishindwa kutimizwa ndani ya
wakati kama ilivyoahidiwa, pasipo kutolewa maelezo yoyote juu ya
kushindwa kutimia kwa ahadi hizo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti tofauti askari na maafisa wa Majeshi
mbalimbali wameelezea masikitiko yao dhidi ya kile walichokiita SIASA
WARIDI kwa kupewa ahadi nzuri na tamu zenye harufu nzuri huku
zikishindwa kutimizwa ndani ya wakati na bila kutolewa maelezo yoyote,
kiasi ambacho askari na maafisa wanabaki wakiishi kwa mategemeo makubwa
huku hakuna kinachotimia.
Askari na Maafisa hao wamelalamikia na kusikitishwa na suala la
kushindwa kuwekewa posho maalumu(package) kama mbadala wa vinywaji na
bidhaa zote zilizokuwa zikipatikana katika maduka yao kwa muda wa miezi
mitano(5) sasa, kama ambavyo imekwisha kutangazwa na Mheshimiwa Rais
katika hafla mbili tofauti za kijeshi, pamoja na Waziri wa Fedha,
Uchumi na Mipango wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni kuwa
posho hiyo itaanza kulipwa kuanzia mwezi July 2016. Lakini mpaka sasa
hakuna malipo yoyote yaliyofanyika.
Nikinukuu maneno ya mmoja wa Maafisa hao alisema;
"Ni aibu na hatari kubwa kwa Taifa kuona sisi askari na maafisa
tukilalamika kupata stahiki zetu, lakini inafika hatua inabidi tupaze
sauti ili ziwafikie wahusika wakuu waweze kutimiza na kutekeleza ahadi
zao. Maana kazi ya ulinzi ni kazi ngumu sana Duniani yenye changamoto
nyingi sana hasa hapa Nchini kwetu Tanzania. Kazi hii inatakiwa ifanyike
kwa uzalendo uliotukuka na kujitoa kwa moyo wote, hivyo kushindwa
kutimiziwa stahiki zetu sisi askari na maafisa kunapunguza hamasa na
moyo wa kazi.
Serikali inapaswa iliangalie suala hili kwa kina zaidi, vinginevyo
linapoza na kushusha hali na mioyo yetu sisi Wazalendo nambari moja hapa
Nchini kwetu Tanzania"
Askari na Maafisa hao wanaiomba Serikali aidha iweze kuwaingizia posho
hiyo au watangaziwe ni mwezi gani itaingizwa rasmi ili wawe timamu
kuingoja kwa muda uliotajwa kuliko kukaa na kusubiri ahadi ya matumaini
bila mafanikio yoyote.
Walinzi wetu hao wamemalizia kwa kusema kwamba wao wapo imara na
hawatarudi nyuma katika kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama Nchini
inazidi kuimalika kila leo na wapo bega kwa bega na Watanzania wote
katika kutimiza majukumu yao.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA