Dar
es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo ametoa ya
moyoni kuhusiana na wanasiasa Kingunge Ngombare Mwiru na Edward Lowassa
akitaka waombwe radhi.
Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako amesema wanasiasa hao
wamekosewa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho amekitaka kiwapigie
magoti Watanzania hao.
Mchungaji huyo amesema hayo katika mahojiano maalumu yaliyofanyika
nyumbani kwake Kawe jijini Dar es Salaam ametumia muda mwingi kueleza
jinsi Lowassa na Kingunge walivyo muhimu kwa CCM.
Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Serikali ya Awamu ya
Nne, na Kingunge ambaye ni mwanasiasa mkongwe aliyefanya kazi kwa karibu
na awamu zote nne za kwanza, walihama CCM wakati wa kuelekea Uchaguzi
Mkuu mwaka jana,
wakipinga uendeshaji mchakato wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.
“Unawezaje kumuacha Mzee Kingunge na Lowassa wakaenda kwenye vyama
vingine? Wale ni asset (mali). Ingekuwa mimi, ningerudi na kumpigia
magoti Mzee Kingunge na kumwambia ‘Mzee chama kinakuhitaji rudi
tukijenge,” amesema.
Mchungaji huyo maarufu amesema CCM imetumia muda mrefu kuwafinyanga viongozi hao, kwa hiyo ni hasara kwa chama kuwaacha.
“Mimi ninachojua ni kuwa Lowassa ni kiongozi mzuri, ana ubinadamu.
Katika watu ambao Mungu alitujalia kuwa viongozi, Lowassa yumo. Hata
uniambie Lowassa mwizi, mimi sikubali,”amesema.
Lusekelo amemsifu Lowassa kuwa ndiye kiongozi pekee ambaye wakati akiwa
Waziri wa Maji alithubutu kuvunja mkataba mbovu wa kampuni ya City Water
iliyoingia mkataba wa kutoa huduma ya maji jijini Dar es Salaam.
“Unawezaje kumtukana mtu, sijui eti ni mgonjwa sijui nini. Hana kosa
yule mtu. Amefanya nini, kwa nini kama Lowassa ni mwizi asikamatwe?
Viongozi wa CCM wangapi ni wezi na ambao tayari wameshakamatwa, lakini
Lowassa hakamatwi?” amehoji.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA