SIMBA imekamatika kwani inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Sh milioni 500 kama malipo ya kodi ya jengo la klabu hiyo lililopo Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
TRA iliwasiliana na Simba hivi karibuni na kuwataka kulipa Sh milioni 500 ikiwa ni malipo ya kodi ya jengo lao hilo ambalo lilikuwa halilipiwi kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Simba wametakiwa kulipa kidogo kidogo kiasi hicho cha fedha hadi watakapomaliza kitakapokamilika.
Katika ulipaji huo wa kidogo kidogo, Simba wametakiwa kulipa kiasi cha Sh milioni 45 kila mwezi ili kuweza kulinusuru jengo lao hilo ambalo ni makao makuu ya klabu hiyo.
Akizungumza na Championi Jumamosi, mmoja wa viongozi wa Simba alisema, kwa sasa klabu hiyo ipo katika wakati mgumu kifedha kutokana na kutakiwa kulipa fedha hizo TRA kila mwezi ili kulinusuru jengo lao.
“Kuna kipindi TRA walikuja kwa ajili ya kudai kodi ya jengo letu lililopo Msimbazi ambayo haijalipwa kwa miaka mingi na kusababisha kufikia kiasi cha Sh milioni 500.
“Tumekubaliana kupeleka kiasi cha Sh milioni 45 kila mwezi tangu kipindi walichotueleza kama miezi mitatu iliyopita hivyo tunaendelea na malipo hayo kila mwezi,” alisema kiongozi huyo.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema yupo likizo na kuelekeza suala kwa ofisa mwingine ambaye hakuwa tayari kulizungumzia jambo hilo.
Source: Global Publisher
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA