Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini DCP Mohamed
Mpinga amesitisha utendaji wa chama cha Kutetea Abiria Taifa (CHAKUA)
kuendelea na shuguli zake katika mikoa yote nchini isipokuwa kwa mkoa wa
Dar es Salaam pekee.
Akitaja sababu za kusitisha utendaji wa chama hicho leo jijini Dar es
Salaam wakati akitoa ripoti ya namna walivyojipanga kuzuia ajali za
Barabarani DCP Mpinga amesema, utendaji mbaya na kukiuka maadili na
kujikita katika usimamizi wa sheria badala ya kutoa elimu unaofanywa na
chama hicho ndiyo sababu ya kusitishwa kwa utendaji wao na kwamba
kuanzia sasa shughuli zao zitafanywa na Mabalozi wa Usalama Barabarani.
Muda mfupi baada ya kutolewa kwa tamko hilo, tulifanikiwa kumpata
Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Kutetea Abiria Taifa, Bwana Hassan
Mchanjama ambaye alikanusha tuhuma hizo huku akisema kuwa, kuzuia
utendaji wa chama cha abiria kwa kile alichokiita ni maslahi binafsi ni
kuwanyima wananchi mahala pa kuwasilisha kero zao ambapo amebainisha
kuwa chama hicho hakijawahi kukiuka taratibu zake za utendaji kama
ilivyoelezwa.
Mbali na suala hilo DCP Mohamed Mpinga amewataka wamiliki wa magari kote
nchini kuondoa na kuacha mara moja kutumia taa zenye mwanga mkali
maarufu kwa jina la 'Sportlights' katika vyombo vyao vya moto kwani taa
hizo ziimekuwa kero kwa madereva wengine na kuchangia ajali za
barabarani nchini.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA