Mwandishi wa kujitegemea wa kituo cha televisheni cha ITV, Halfani
Lihundi ameachiwa kwa dhamana kutoka katika kituo cha Polisi cha
Changamoto, Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha alikokuwa
anashikiliwa tangu juzi, na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Desemba 27,
mwaka huu.
Alikuwa anashikiliwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander
Mnyeti, baada ya kuripoti habari inayoelezwa na mkuu huyo wa wilaya kuwa
haikuwa sawa na kuamuru kukamatwa kisha, kulala mahabusu na hatimaye
kufanikiwa kutoka jana saa tisa alasiri.
Awali, waandishi wa habari wa Arusha walikusanyika kituoni hapo ili
kujua hatma ya mwenzao na baadaye kuamua kwenda kumuona Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ili kumweleza kuwa
mwenzao amekamatwa kwa sababu ya migogoro ya wananchi.
Wakati Lukuvi anatoka kwenye kikao cha kujadili migogoro ya ardhi
kilichofanyika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, waandishi waliimba
wimbo wenye lengo la kufikisha ujumbe kuwa, wanataka wenzao aachiwe
huru. Waliimba; “Solidarity Forever, Bring Back Halfani Lihundi.”
Lukuvi alisema hahusiki na suala hilo na kuwasihi wanahabari kwenda naye
Usa River kwenye mkutano ambapo Mnyeti atatoa tamko juu ya suala hilo.
Lakini Mnyeti alipokuwa akitoka kikaoni hapo aliulizwa na waandishi
kuhusu suala hilo na kosa lipi limefanya Lihundi kushikiliwa Polisi,
lakini hakuzungumza chochote na kuelekea kwenye gari lake kusubiri
msafara wa Lukuvi.
Awali, ilidaiwa kuwa Mnyeti ndiye aliyeamuru Lihundi akamatwe kwa madai
ya kuandika habari za uchochezi za kijiji cha Leguruki, Arumeru.
Alisema alipotaka kujua kosa analoshitakiwa nalo Lihundi, alijibiwa hana
kosa ila yupo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya. Hata hivyo, RB ya Polisi Usa
River 4763/2016 inaonesha ana kosa la uchochezi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA