Trump asisitiza udharura wa Marekani kuimarisha silaha za nyuklia

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump Alkhamisi ya jana alitangaza kuwa, nchi hiyo inapaswa kuimarisha zaidi uwezo wake wa silaha za nyuklia maadamu ulimwengu haujapata mwelekeo wa kimantiki kuhusu silaha za atomiki. 
Donald Trump hakutoa maelezo zaidi katika uwanja huo lakini msemaji wake, Jason Miller amesema kuwa, rais huyo mteule wa Marekani alikuwa akiashiria vitisho vinavyohusiana na uzalishaji na uenezaji wa silaha za nyuklia na udharura wa kukabiliana na vitisho hivyo hususan vile vya makundi ya kigaidi katika maeneo yenye machafuko na "serikali au tawala kigaidi". 

Jason Miller


Trump pia ametilia mkazo suala la kusasisha uwezo wa nyuklia wa kuzuia vitisho kabla ya kutendeka kama mojawapo ya njia muhimu za kuimarisha amani.
Matamshi hayo ni ya kwanza rasmi kutolewa na rais mteule wa Marekani kuhusu silaha za nyuklia za nchi hiyo. Kutangazwa mtazamo huo wa Trump sambamba na matamshi yaliyotolewa na Rais Vladimir Putin wa Russia kuhusu uwezo wa silaha za nyuklia wa nchi hiyo ni jambo linalipaswa kupewa mazingatio maalumu.
Alkhamisi wiki hii pia Rais Putin alitilia mkazo udharura wa kuimarishwa uwezo wa silaha za nyuklia na silaha za kistratejia za Russia na akasema Moscow inapaswa kuimarisha zaidi makombora yenye uwezo wa kufumua na kupasua mfumo wa kujikinga na makombora.
Taasisi za ulinzi za Marekani na Russia zinasema kuwa, nchi hizo mbili pekee ndizo nguvu mbili za nyuklia zinazomiliki silaha za kistratejia za nyuklia katika nyanja tatu za anga, nchi kavu na baharini na kwa sasa zinasasisha zilaha hizo. Wakati huo huo wataalamu wanasema kuwa, inatazamiwa kuwa hadi kufikia mwanzoni mwa muongo wa 2040 Marekani itakuwa imesasisha na kuboresha silaha zake za anga, nchi kavu na baharini za nyuklia kwa kutumia gharama ya dola trilioni moja. Silaha za nyuklia za kipindi cha Vita Baridi zingali sehemu muhimu sana ya stratejia ya ulinzi ya Marekani na maafisa wa nchi hiyo wanasisitiza udharura wa kulindwa uwezo wa nyuklia wa nchi hiyo.

Inaonekana kuwa Marekani ambayo imekuwa ikidai kwamba, inafanya jitihada za kupunguza silaha za nyuklia kote duniani, sasa inaiweka dunia katika ncha ya vita vya nyuklia baada ya maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo katika kipindi cha utawala wa Barack Obama kusisitiza tena sera ya Washington ya kufanya mashambulizi ya mapema ya silaha za nyuklia na sisitizo la sasa la rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump la kuimarisha na kupanua zaidi uwezo wa nyuklia wa Marekani. Katika uwanja huo Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter amesema waziwazi kwamba, Washington itadumisha stratejia ya kufanya mashambulizi ya mapema ya nyuklia, suala mabalo lina maana ya kendelea kuwepo wingu la uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya nyuklia duniani na ni vitisho vya waziwazi dhidi ya nchi nyingine hususan zile zinazomiliki silaha za nyuklia kama Russia na China. Mwezi Juni mwaka jana pia Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert O. Work alisema kuna uhuhimu na udharura wa kuwepo nguvu kubwa ya silaha za nyuklia kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa wa Marekani na kwamba suala hilo linapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza cha Wizara ya Ulinzi. 
Katika sera yake ya mshambulizi ya mapema ya silaha za nyuklia, Marekani imekuwa ikitekeleza mipango kabambe ya kusasisha na kuboresha zaidi silaha zake za atomiki. Hayo yanafanyika kwa kutumia visingizio mbalimbali kama vile usasishaji wa silaha za nyuklia katika nchi wapinzani wa Washington hususan Russia na China ambazo zote mbili hasahasa Russia, zimetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kusasisha silaha zao za kistratejia za nyuklia. Rusia imeazimia kusasisha na kuboresha asilimia 70 ya silaha zake za atomiki hadi kufikia mwaka 2020. Hata hivyo ikilinganishwa na Russia, Marekani ina mipango mikubwa na mipana zaidi ya kusasisha na kupanua zaidi maghala yake ya silaha za nyuklia. 

Marekani ndiyo nchi pekee iliyotumia silaha za nyuklia kuua watu. Hiroshina na Nagasaki, Japan

Kwa kila hali, kwa sasa na hasa baada ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump kutilia mkazo udhaura wa kuimarishwa zaidi uwezo wa silaha za nyuklia wa nchi hiyo inatarajiwa kuwa, sera na mipango ya kupanua na kusasisha silaha za nyuklia za Marekani inashika kasi kubwa zaidi katika kipindi cha Trump, suala ambalo, badala ya kuimaisha amani, linaisogeza zaidi dunia katika ncha ya maangamizi ya silaha hatari za atomiki.  

Chapisha Maoni

0 Maoni