Tundu Lissu ang'ang'aniwa Kisutu

LICHA ya utetezi wa kutaka kuondolewa kwa shitaka la kwanza na tano uliofanywa na wakili wake katika kesi ya uchochezi kwenye Gazeti la Mawio inayomuhusu Tundu Lissu, Jabir Idrissa, Simon Mkina na Ismail Mahaboob, mashtaka hayo wamesomewa leo,


Awali mawakili wa utetezi walitaka shitaka la kwanza na tano kutosomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai kuwa, yanaupungufu kisheria ikiwa ni pamoja na kukosa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singiuda Mashariki , Simon Mkina Mhariri wa Gazeti la Mawio, Jabir Idrissa – mwandishi mwandamizi wa gazeti hilo na Ismail Mahboob ni Meneja wa kampuni ya uchapishaji ya Flint tarehe 19, Juni 2016 walishitakiwa na Jamhuri kwa madai ya kufanya uchochezi kwa kuchapisha habari iliyobeba kichwa cha maneno “Machafuko yaja Zanzibar” tarehe 14-20 Januari 2016, Toleo Na. 182.

Tarehe 20 Septemba 2016, mahamkama hiyo ilitoa uamuzi wa pingamizi hilo ambapo upande wa jamhuri uliambiwa kuwa unauwezo wa kurudisha upya mashtaka hayo.

Leo Patrick Mwita wakili wa serikali mbele Thomas Simba Hakimu Mkazi Mkuu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, amesoma shitaka la kwanza na tano.

Mwita amedai kuwa shitaka la kwanza ni la kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa linalodaiwa kutendwa kati ya tarehe 12 na 14 Januari mwaka huu ambapo;

Idrissa, Mkina na Lissu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam walipanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi.

Katika kosa la tano, mshitakiwa namba moja (Idrissa), namba mbili (Mkina) na namba nne (Lissu), wanatuhumiwa kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa kuchapisha habari “Machafuko yaja Zanzibar” na kwamba, ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.

Mashtaka hayo yalikuwa yanapingwa na mawakili wa upande wa utetezi kwa hoja ya kuwa na upongufu wa kisheria ikiwa pamoja na kutokuwa na kibali cha mwendesha mashtaka wa serikali.

Awali upande wa Jamhuri ulilazimika kusoma mashitaka matatu ambalo ni la pili, tatu na nne.
Shitaka pili likimkabili Jabir, Mkina na Lissu, wakidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti la MAWIO, toleo Na. 182 la tarehe 14-20 Januari 2016.

Shitaka la tatu linamuhusu Ismail akidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti hilo lenye kichwa cha Habari ‘Machafuko yaja Z’bar’.

Shitaka la nne linamkabili Ismail akidaiwa kuchapisha gazeti bila kupeleka kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Upande wa Jamhuri umedai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo wameiomba mahakama ipange tarehe ya usikilizwaji wa awali. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 18 mwezi mosi mwaka 2017.

Chapisha Maoni

0 Maoni