CUF ya Maalimu Seif, Prof Lipumba kubainika leo

Siku chache baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutengua Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Prof. Ibrahim Lipumba, leo mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi mwingine kuhusu hatima ya uenyekiti wake.

Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Shauri hilo namba 23 la mwaka 2016, lililofunguliwa na chama hicho upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, linatarajiwa kutolewa uamuzi leo mbele ya Jaji Benhajj Masoud wa Mahakama Kuu, baada ya awali kushindwa kusikilizwa na Jaji Wilfred Dyansobera aliyehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti 2015, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa madai kuwa haungi mkono makubaliano yaliyofikiwa na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Prof. Lipumba alichukua uamuzi huo baada ya vyama hivyo kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea wao wa urais.

Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye Prof. Lipumba alimwandikia barua Katibu Mkuu, Maalim Seif, akiomba kurudi katika nafasi yake.

“Nimemwandikia Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) kutengua barua yangu niliyoandika tarehe 5 Agosti, mwaka 2015. Sasa nasubiri majibu kutoka kwa Katibu Mkuu baada ya barua yangu kujadiliwa na ngazi husika za chama,” alisema Lipumba kwenye barua yake ya wakati huo.

Ombi hilo la Prof. Lipumba lilikataliwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho hasa wanaomuunga mkono Maalim Seif, hivyo kusababisha mgawanyiko kati ya wanachama wanaomuunga mkono profesa huyo wa uchumi na wale wanaomuunga mkono Maalim Seif.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alitangaza kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti halali wa (CUF), jambo lililopingwa vikali na baadhi ya wanachama wa chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu.

Mtafaruku huo ndio uliosababisha kufunguliwa kwa kesi ya kikatiba na kambi ya Maalim Seif kupinga uenyekiti wa Prof. Lipumba.
 
Tangu kurejea kwake kama mwenyekiti wa chama hicho, kumekuwa na mgawanyiko na mivutano baina ya viongozi na wanachama wa chama hicho.

Hali hiyo ilisababisha hata baadhi ya wabunge wa chama hicho kujiuzulu na wengine kutenguliwa ubunge wao baada ya mwenyekiti huyo kuteua wabunge wapya wa kambi yake.

Chapisha Maoni

0 Maoni