UFAFANUZI WA MANENO CHRISTMAS NA X-MAS
Kwa leo nina jambo moja la kuweka sawa. Vijana kadhaa wameniomba nitoe
maelezo kuhusiana na maneno “CHRISTMAS” na “X-MAS” maana wanachanganywa
na wenzao. Kifupi, maelezo yanayosambazwa kwenye mitandao yetu ni kwamba
“Christmas” ni sahihi na “X-mas” siyo sahihi. Maelezo haya
yanayosambazwa si sahihi, ni ya uongo.
Tukianzia kwenye maneno hayo, kwa karibu kabisa tunarudi kwenye maneno
ya lugha ya Kiingereza cha enzi tatu: Kiingereza cha zamani, Kiingereza
cha enzi ya miaka ya kati (karne 5 hadi15) na Kiingereza cha siku hizi.
Kwa Kiingereza cha zamani “Christmas” ilitamkwa “Cristes maesse” na
maana yake ilikuwa “Christ’s festival” yaani sikukuu ya Kristo.
“Crist” ndiyo “Christ” ndiyo Kristo. Kristo maana yake “Mpakwa” ndiyo
inayotafsiri jina la Kiebrania (lugha ya Wayahudi) “Meshiah”, yaani
“Mpakwa wa Bwana” . “Meshiah” ndiyo tunayotamka sisi Waswahili kama
Masiya au Masiha.
Neno “maesse” maana yake “festival” yaani sikukuu au sherehe. Katika
Kiingereza za enzi ya kati “Cristes maesse” ilinyooshwa na kuwa
“Cristemas” ndipo katika Kiingereza cha siku hizi ikafika kutamkwa na
kuandikwa “Christmass”.
Yaani hapa tunacheza na maendeleo ya lugha ya Kiingereza katika matamshi na maandishi tu. Hadi hapo nadhani nimeeleweka.
Lakini suala la CHRISTMAS na X-MAS linarudi kwenye lugha ya Agano Jipya
ndiyo Kigiriki au Kiyunani. Jina hilo “Crist” au “Christ” limetoholewa
kutoka jina “CHRISTOS” ndiyo Kristo (tukifupisha kwa kudondosha “s” ya
mwishoni).
Walatini (watu wa Dola ya Rumi) wakatamka “CHRISTUS” ndiyo Kristu
(tukifupisha kwa kudondosha “s” ya mwishoni). “Christos” maana yake ni
Mpakwa, Masiya au Masiha. Masiya au Masiha yenyewe inatoholewa kutoka
jina la Kiebrania “Meshiah” kama nilivyoonesha hapo juu. Waingereza
hutohoa “Meshiah” na kuandika na kutamka “Messiah”.
Kumbe katika Kigiriki au Kiyunani, “CHRISTOS” huandikwa kwa herufi ndogo
"Χριστός” na kwa herufi kubwa “XPICTOC” au “ΧPIΣTOΣ” au kwa sanaa
“XPISTOS”. Katika Kigiriki hiyo “X” siyo “eksi” bali ni “ch” na hiyo “P”
siyo “pi” bali “r”. Hivi kwa Kigiriki “XPI” husomwa “Chri.”
Halafu, kutokana na herufi “X” na “P” kusimama mwanzoni mwa jina
“XPISTOS” au "XPICTOC", Wakristo wa mwanzo walizitumia herufi hizo mbili
kufupisha jina “CHRISTOS” hivyo wakawa wanaandika wakibebanisha “X” na
“P” na kuzaa alama moja maarufu sana mnayozoea kuiona kwenye nguo za
misa au vitambaa vya altareni na kwenye vitabu. Ni alama ya “P”
iliyokatwa mguuni kwa mstari -- au X.
(Poleni, hapa nashindwa kuichora. Herufi za Kigiriki zinagoma).Alama hizi huwa altaren,katika mavazi na vifaa vya kanisa.
Kwa maelezo haya basi, “X-MAS” si neno tofauti na “CHRISTMAS”. Ni neno
lile lile isipokuwa badala ya kuandika CHRIST kirefu watu wanafupisha
kwa X tu. Ndipo inapotokea X-MAS mahali pa CHRISTMAS. Hivyo hiyo “X” ya
mwanzoni haimaanishi “mkasi” wenye maana ya “kukata” au “hakuna” bali
“X” yenye kufupisha jina “CHRISTOS” na “MAS” huko mwishoni kumaanisha
“SIKUKUU” au “SHEREHE”.
Kwa hiyo, asiwadanganyeni mtu wala asiwababaisheni mtu kwamba “X-MAS”
maana yake “HAKUNA KUSANYIKO LA KRISTO” eti kwa vile “MAS” ni neno la
Kigiriki linalomaanisha “MKUSANYIKO”. Hakuna neno la Kigiriki MAS
linalomaanisha MKUSANYIKO.
Iweni na amani, vijana. Hata mtu akilazimisha maneno ya Kigiriki maneno
yote yanayokaribiana na MAS japo kwa maandishi na matamshi hakuna neno
lenye maana ya mkusanyoko.
Tazama maneno yaliyopo ni “μασάομαι” lenye maana ya kuuma, kung’ata,
“μαστιγόω”lenye maana ya mchapo wa kiboko au kuadhibu, “μαστίζω”lenye
maana ya kuchapa, “μάστιξ” lenye maana ya pigo la mjeledi na maradhi na
“μαστός” lenye maana ya kifua.
Kama msomavyo hapa katika maneno haya hakuna neno linalomaanisha “MKUSANYIKO”.
Basi, vijana kuweni na amani. X-MAS si neno tofauti na CHRISTMAS. Ni
neno lile lile isipokuwa badala ya kuandika CHRIST kwa urefu watu
wanafupisha kwa X tu.
Nawatakieni maandalizi mema ya Krismasi au Noeli.
Kwisha kumaliza somo hili la lugha ya Kiingereza na Kigiriki naomba kuwaongezea mambo kidogo.
Majina: sikukuu hii huitwa pia Kuzaliwa (Nativity) au Yule.
Ni sikukuu ya utamaduni wa Kikristo. Maana yake ni kukumbuka na
kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Na kwa vile ni shauri la Mungu
kutupatia sisi wakosefu zawadi ya Mkombozi, katika kuadhimisha sikukuu
hii zawadi hutawala. Ni sikukuu inayosherehekewa kwa mikusanyiko,
upambaji wenye ishara nyingi kama vile miti ya Krismasi na dhifa za
keki, kula na kunywa pamoja.
Tarehe ya kuadhimisha katika Kanisa la Magharibi na baadhi ya Makanisa
ya Mashariki pamoja na walimwengu wengine ni tarehe 25 Desemba. Lakini
katika baadhi ya Makanisa ya Mashariki huadhimishwa tarehe 7 Januari. Na
katika makanisa ya Kiarmeni huadhimishwa tarehe 6 Januari.
KILA LA HERI KWENU NYOTE!
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA