POLISI mkoani Morogoro imewafikisha mahakamani watu saba kati ya 12, kujibu tuhuma za kumjeruhi kwa kumchoma mkuki mdomoni hadi kutokea shingoni, Augustino Mtitu (35).
Walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa huku wengine watano, wote wakazi wa kitongoji cha Upangwa wilayani Kilosa wakisubiri kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana alipokuwa anazungumzia msako uliofanywa na polisi na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao baada ya kutokea kwa tukio hilo Desemba 25, mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi eneo la kitongoji cha Upangwa, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata na Tarafa ya Masanze wilayani Kilosa.
Kamanda Matei alisema katika msako huo, watu 12 walikamatwa na saba kati yao tayari wamefikishwa mahakamani. Wengine watano watafikisha mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Hata hivyo, Kamanda huyo aliwataja majeruhi wa tukio hilo mbali na Mtitu ambaye bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kuwa ni George Andrew (68) aliyejeruhiwa kichwani.
Wengine ni Yohana Wisa (26) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Mathayo Elia (34) aliyejeruhiwa kichwani na bega la kushoto, Josephat Mtitu (55) aliyejeruhiwa begani na shavuni na mwingine ni Paulo Thomas (56) aliyejeruhiwa mbavu na mkono wa kushoto.
Wote ni wakazi wa kijiji cha Dodoma Isanga na wanaendelea vizuri. Hivi karibuni, baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai waliwashambulia kwa silaha za jadi na kuwajeruhi watu sita akiwemo Mtitu mara baada ya kukamata mifugo ya mtu mmoja aitwaye Ngoyoni Kimang’ati, iliyokuwa ikiharibu mahindi shambani.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA