Wavuvi 13 wa kutumia mabomu wanaswa feri

UONGOZI wa Soko la Samaki la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam umewakamata watu 13 wanaohusishwa kuvua shehena ya samaki 473 karibia tani 1.3 wenye thamani ya Sh milioni 13 kwa kutumia mabomu.


Samaki hao aina ya kolekole, jodari, changu, pono, sehewa na nguru waliingizwa sokoni hapo Desemba 16, mwaka huu na baada ya ukaguzi, ikabainika kuingizwa kwa samaki hao, huku wahusika wakidaiwa kutoroka.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya soko hilo, kupitia upya mfumo wa mapokezi, ulinzi na usimamizi ili kujiridhisha kama uko safi. Kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa hao,

Meneja wa Soko hilo, Eliakim Mniko alisema jana kuwa, walikamatwa sokoni hapo na wamefikishwa polisi kutoa maelezo na kufunguliwa kesi itakayoanza kusikilizwa mapema mwakani.

Akiwa katika ziara sokoni hapo Desemba 19, 2016, Dk Tizeba alisema ni aibu kwa kitendo hicho kufanyika meta chache kufika Ikulu na kwamba kama suala la ukaguzi limewashinda, Bodi ya soko iachie jukumu hilo kwa mamlaka nyingine ifanye kazi sokoni hapo.

Pia aliagiza wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kutangazwa kuwa ndio wanaoharamisha uvuvi na kulitia hasara taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni