MATAMBIKO ASILI YA TAMTHILIA...

Je, wajua kuwa matambiko ni asili ya tamthilia za leo kama unazozifahamu? Je, unafahamu kuwa matambiko yalikuwepo toka enzi za kale na si Afrika pekee yake? Je, unaamini katika matambiko ya kwenu? Kwa nini?
Kuna chunguzi mbalimbali ambazo zimefanya tafiti nyingi ili kujua asili ya tamthilia ambazo leo hii tunakaa kwenye luninga na kufurahia kuzitazama kama tamthilia za kina Kanumba, Ramsey, Van Vica na zingine nyingi, lakini
cha ajabu ni kuwa, hakuna anayejua muda sahihi ni lini tamthilia hizi zilianza. Kutoka na kuwa na ugumu wa kujua muda stahiki wa kuzaliwa kwa tamthilia, zipo nadharia anuai ambazo wanafasihi wamezitumia kama ni chanzo cha kuzaliwa kwa tamthilia. Nadharia moja wapo ni NADHARIA YA MATAMBIKO (RITUAL THEORY).
MATAMBIKO NI NINI?
Matambiko ni shughuli maalumu za kijamii zinazofanywa kwa
hatua na kila hatua ina maana halisi katika matambiko hayo. Shughuli hizi hufanywa na jamii Fulani kwa kuongozwa na mkuu wa jamii hiyo, na shughuli hizo hufanyika kiimani zaidi. Matambiko haya lazima yawe na wahusika ambapo mhusika mkuu ni mganga wa kienyeji  Zipo aina mbalimbali za matambiko, lakini katika makala hii nimekuandalia aina tatu kama ifuatavyo.
1.      1   Matambiko ya kuhama hatua Fulani katika maisha (Life crisis ritual).
Katika matambiko haya, jamii humsaidia kijana kuchukua hatua au kuhama hatua Fulani katika maisha. Ikumbukwe kuwa, kila aina ya tambiko linakuwa na kazi yake na matambik hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Katika aina hii ya tambiko, kijana/binti hufundishwa mambo kadha wa kadha ya maisha. Mfano mzuri ni unyago, jando na kadhalika. Katika unyago, binti hufundishwa namna ya kuwa mama sahihi wa familia na mke halisi wa mume, mafundisho ambayo isku hizi yamebadilishwa na kuwa kitchen party na mambo ambayo hufanyika kwenye kitchen party ni sawa sawa kabisa na mambo yaliyokuwa yanafanyika kwenye unyago.
2.     2  Matambiko ya kujikabidhi katika ulimwengu mwingine.
Haya ni matambiko ambayo hufanyika kwa lengo la kujikabidhi maksudi katika ulimwengu mwingine, ambapo watu hunyenyekea nguvu Fulani ambayo wanaamini ndo msaada kwao. Aina hii ya matambiko hufanyika wakati jamii inapokabiliwa na tatizo la aina Fulani kama ukame, njaa, mauaji, mmomonyoko wa maadili na kadhalika. Katika tambiko hili, watu hufanya sherehe maalumu kwa kuchinja wanyama wa aina Fulani ili kuiridhisha nguvu waiaminiyo. Siku hizi, aina hii ya tambiko inafanywa hata kwenye makanisa, ambapo wakristo huuita ushirika na kwa imani ya kiislamu, huita dua maalumu.
3.       3Tambiko maalumu (redress ritual).
Hii ni aina nyingine ya tambiko ambalo hufanyika kwa lengo maalumu endapo kuna mtu Fulani katika jamii anakabiliwa na tatizo la kimaisha. Tambiko hili huweza kufanyika kwa ngazi ya familia na mtu ambaye anakabiliwa na tatizo huandaa mazingira ya aina yake ambapo tambiko hilo hufanyika.
KWA NIN TAMBIKO NI ASILI YA TAMTHILIA?
Inaaminika kuwa, asili ya tamthilia, ni tambiko, na tambiko ni tamthilia. Hii ni kutokana na vitu ambavyo hupatikana kwenye tambiko, ambavyo pia ni msingi wa tamthilia yoyote. Mambo makuu nay a muhimu katika tambiko ni manne, ambayo ni: madhari, mtindo, dhamira na fanani.
Tambiko lolote lazima liwe na sehemu maalumu ya kufanyika, sehemu ambayo huchaguliwa ili tukio hilo lifanyike kwa uhalisia kama porini, njia panda na kadhalika. Tambiko pia lazima liwe na mtindo, yaani ni jinsi gani litafanyika. Yapo matambiko ambayo huwataka wahusika wakae mikao Fulani, au wakati mwingine tambiko lifanyike wahusika wakiwa uchi.
Tambiko pia lazima liwe na dhamira/dhima. Kuna matambiko yanayofanyika maalumu kwa ajili ya kuomba mvua, kuomba hali ya mazao iwe nzuri, na kadhalika.
Lakini pia, kila tambiko lina fanani, yaani watu wanaoshuhudia tukio lenyewe.
Mambo haya manne ni msingi wa tamthilia, tamthilia ambayo leo hii imekufanya usahau asili yako. Je, wewe unafahamu asili yako ni tambiko la aina gani? Upo tayari sasa kulifanya ili turejee katika asili yetu? Au huwezi kufanya tena tambiko kwa sababu umeelimika umebahatika kupata stashada au shahada, pengine zaidi ya hapo? Je, unajua wazungu wametuvisha ujinga ambao mimi na wewe ni lazima tuamke kurejea kwenye asili?
BADILIKA LEO, TAMBIKO NI ASILI YAKO.

Chapisha Maoni

0 Maoni