Leo
ningependa kuendelea na uchambuzi wangu wa siasa za Tanzania na hatima ya
maendeleo ya nchi kama ilivyo ada ya ukurasa huu wa blog. Kikubwa ambacho
ningependa leo kuchangia katika ukurasa huu ni juu ya sera mbalimbali za
maendeleo na madhara ya siasa katika utekelezaji wa sera hizo. Pamoja na hilo,
ningependa pia ndugu msomaji wangu wa makala hii utambue kuwa, siasa ni kila
kitu katika maisha ya kila siku kama
nilivyosema kwenye mada yangu ya wiki
iliyopita. Bila shaka utakumbuka vizuri niliongea masuala anuai yanayogusa
utawala na masuala anuai ya kimaendeleo. Songa na mimi katika mada hii.
Kwanza
kabisa nitumie fursa hii kuwashukuru wachangiaji wangu ambao pia wamenitia moyo
kwa dhati kabisa katika kuendeleza uchambuzi wa masuala haya ambayo pia yanalenga
mustakabali wa maisha yetu kama watanzania kwa ujumla wetu.
Sera
ambayo ningependa kuanza nayo ni sera ya elimu ambayo imekuwa ikipigiwa kelele
kila siku na wadau mbalimbali wa masuala ya elimu na hivyo kukosa muafaka
halisi wa namna gani sera hii iwezeshwe kuwa yenye tija katika maisha ya
watanzania walio wengi na imwandae pia mtanzania katika soko la ushindani la
ajira Afrika na ulimwenguni kote. Pembeni yangu ninayo sera ya Elimu ya mwaka
2014 ambayo imebainisha mambo mbalimbali ya msingi kabisa yenye lengo la kupiga
hatua katika kile ambacho watunga sera wanaamini kuwa ni mtumbwi wa kuwasukuma
watanzania kuelekea katika nchi yenye uchumi wa kati.
Kabla
sijaenda mbali, nipende tu kuwakumbusha pia, sera yetu inaamini katika mfumo wa
2+7+4+2+3+, yaani, miaka miwili katika shule ya awali, ama chekechea, miaka
saba ya elimu ya msingi, miaka mine ya shule ya upili (secondary), miaka miwili
ya shule ya upili mwendelezo (Advanced secondary) na miaka mitatu na zaidi
katika elimu ya chuo, kama ulivyoainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya
ufundi Ukurasa wa 21.
Nini
Tamko la serikali kwa elimu ya awali?
Nimeona
tuanzie na matamko ya serikali katika mfumo huu ambao kimsingi mlengo mahsusi
wa elimu yetu. Tamko la serikali kwenye elimy ya awali (chekechea) ni kama
lifuatalo;
“Serikali itaweka utaratibu
wa elimu ya awali kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto wenye umri kati ya
miaka mitatu hadi mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja” (T.I.E, 2014)
Kwa
kawaida sera ya elimu ya awali kufanywa kuwa ya lazima ni jambo la msingi,
lakini hofu yangu ni kwamba, je, ni mazingira gani ambayo mtoto atawekewa ili
kumtengenezea uwezo na uelewa pamoja na kumjengea msingi imara wa kitaaluma ili
aweze kuendela vema na viwango vingine zaidi vitakavyofuatia?
Tafsiri
yangu ya msingi ni kwamba, je serikali imeandaa nini maalumu kwa watoto
wanaoanza na shule hii ya awali ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na vitu?
Umri uliotajwa kiukweli kabisa na kifalsafa ni halisi kwa mtoto kujifunza vitu
vyepesi vyepesi hasa kwa njia ya michezo, kama alivyowahi kueleza mwanafalsafa Jacques
Rossoeau, ambapo anaamini kwamba, katika hali ya kawaida na umri wa kuanzia
miaka 0-5, mtoto anatakiwa ajifunze vitu vya kawaida kwa njia ya michezo na
kuimba ambayo itamjengea uelewa. Swali hapa ni je, mazingira ya michezo kwa
mtoto, serikali imejipangaje, ikiwa ni pamoja na bembea mashuleni maalumu kwa
ajili ya hiyo michezo, au tu kwa kucheza chini na kuchimbachimba ndo serikali
imejidhatiti kutoa kwa watoto hawa?
Ushauri
wangu, dhana ya Elimu bure ianzie kwenye elimu ya awali, elimu ambayo huwa ni
msingi wa mengine yote yanayofuatia baada ya hapo na ambayo mtoto hufanya kama
chanzo cha maarifa mengine.
Lakini
pia, serikali ione utaratibu wa kuanzisha elimu amaalumu kwa ajili ya kuandaa
rasilimali watu:rasilimali ambayo itakuwa maalumu kwa ajili ya watoto. Hii ni
kutokana kuwa, kwa rasilimali ambazo zinatoka vyuoni moja kwa moja naamini
hazina uelewa halisi wa malezi kwa watoto wenye umri mdogo kama huu uliowekwa
na serikali. Hivyo basi, ni vema kwa nia ya dhati kabisa serikali itabaini ni
sehemu gani mahsusi kwa ajili ya kuzalisha rasilimali watu ya kutosha kwa ajili
ya kuzalisha na kuanzisha msingi imara katika taaluma ya mtoto.
Itaendelea…
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA