Waziri Muhongo akutana na waingereza wenye nia ya kuzalisha umeme nchini


 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia), akiwasikiliza Viongozi Waandamizi kutoka Kampuni ya ‘Solar Securities’ ya Uingereza, Nicholas Richardson ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji (katikati) na Manoli Yannaghas – Mkurugenzi (kushoto); walipomtembelea ofisini kwake hivi karibuni kwa lengo la kuonesha nia yao ya kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akisisitiza jambo katika kikao baina yake na Ujumbe kutoka Kampuni inayojishughulisha na masuala ya nishati mbadala kutoka Uingereza, ‘Solar Securities (hawapo pichani)
 Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele (kulia), akifurahia jambo wakati wa kikao baina ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Ujumbe kutoka Kampuni inayojishughulisha na masuala ya nishati mbadala kutoka Uingereza, ‘Solar Securities (hawapo pichani). Masele ni mshirika wa Kampuni hiyo. Kulia ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Nishati Mbadala, Jacob Mayala.

Kutoka Kulia ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Nishati Mbadala, Jacob Mayala, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Solar Securities Nicholas Richardson, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Manoli Yannaghas, Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, wakiwa katika kikao ambacho Ujumbe kutoka Kampuni husika ulionesha nia kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini.





Kutoka Kulia ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Nishati Mbadala, Jacob Mayala, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Solar Securities Nicholas Richardson, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Manoli Yannaghas, Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, wakiwa katika kikao ambacho Ujumbe kutoka Kampuni husika ulionesha nia kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini.



Na Veronica Simba
Ujumbe kutoka Kampuni inayojishughulisha na masuala ya nishati mbadala kutoka Uingereza, ‘Solar Securities’, umemtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo kuhusu nia yao ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati hapa nchini.
Viongozi waandamizi kutoka Kampuni hiyo, Nicholas Richardson (Mkurugenzi Mtendaji) na Manoli Yannaghas (Mkurugenzi), walimweleza Waziri Muhongo kuwa lengo lao ni kuwekeza nchini kwa kuzalisha umeme wa jua.
Akitoa mwongozo wa nia iliyowasilishwa na Ujumbe huo, Profesa Muhongo aliwaeleza kuwa, Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa uwekezaji nchini hususan katika sekta ya nishati, ambapo wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza watashindanishwa kwa uwazi na wale watakaokidhi vigezo ndiyo watapata fursa ya kuwekeza.
Alisema kuwa, kwa kuanzia, mwongozo wa utaratibu huo mpya kwa upande wa sekta ndogo ya gesi na mafuta uko mbioni kukamilika na utafuatiwa na miongozo husika kwa sekta nyingine za nishati.
Alitumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza katika sekta husika kuutumia ipasavyo mwongozo husika pindi utakapokuwa tayari ambapo alisema utasambazwa duniani kote ili waweze kuelewa vyema fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
 Vilevile, alieleza kuwa, Serikali hususan wizara yake, imefanya mabadiliko katika utaratibu wa majadiliano baina yake na wawekezaji wanaoonesha nia za kuwekeza nchini, ambapo sasa majadiliano yatatumia muda mfupi tofauti na ilivyokuwa zamani ili kuleta tija kwa pande zote mbili.
“Awali, tulikuwa tukipoteza muda mrefu katika majadiliano. Sasa majadiliano yanachukua muda mfupi na kufikia makubaliano,” alisisitiza.

Profesa Muhongo alimwagiza Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, kufuata utaratibu huo wenye kutumia muda mfupi kwa kuandaa kikao kitakachohusisha pande zote likiwemo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na wataalam kutoka wizarani, kujadili maombi yaliyowasilishwa na Kampuni hiyo ili kufikia muafaka ndani ya muda mfupi.

Chapisha Maoni

0 Maoni