Hivi ndivyo sakata la madawa ya kulevya lilivyomnufaisha Makonda


Baada ya kuja na operesheni ya kupambana na dawa za kulevya, jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda linaweza kuwa ndilo lililotajwa zaidi katika mkutano wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita na kwenye mitandao ya kijamii kwa wiki ya pili sasa.

Makonda alianza kuwa mjadala ndani na nje ya nchi baada ya kutaja orodha ya kwanza na ya pili ya watu maarufu wakiwamo wasanii, wanasiasa na viongozi wa dini na kuagiza wafike Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam wahojiwe kuhusu dawa za kulevya.

Kasi ya kutajwa kwa jina lake iliongezeka zaidi Jumatano iliyopita baada ya kumtaja Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, Askofu Josephat Gwajima na mfanyabiashara Yusuf Manji.

Hata hivyo, Mbowe, Gwajima na Manji wamekanusha vikali kuhusika na biashara hizo na kuahidi kumshtaki Makonda kwa kashfa. Gwajima na Manji wameshahojiwa polisi.

Katika mtandao wa kijamii wa JamiiForums, hadi kufikia juzi saa 8:00 mchana, kulikuwa na kurasa 49 ambazo jina la Makonda lilikuwa limetajwa mara 961 katika mijadala iliyokuwa ikiendelea.

Mijadala hiyo ilikuwa ikihusu kama Makonda yuko sahihi au la katika utaratibu alioutumia na kama ana mamlaka ya kuagiza watu kuripoti polisi.

Chapisha Maoni

0 Maoni