Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhandisi Tumaini Magesa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tamim Kambona, kwenda kata ya Engusero keshokutwa kujibu kero za wananchi katika mkutano wa hadhara.
Mkuu huyo wa wilaya na mkurugenzi wametakiwa wafuatane na Mwenyekiti wa Halmashauri, Lairumbe Mollel kwenda kuitisha mkutano huo.
Majaliwa alitoa maagizo hayo jana katika kijiji cha Engusero baada ya kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mji wa Kibaya, yalipo makao makuu ya wilaya hiyo kuanza ziara ya kikazi ya mkoa wa Manyara.
Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na wananchi wa Engusero, Waziri Mkuu alisema analichukua na kwenda kulifanyia kazi ombi la wakazi hao la kujengewa soko la kimataifa katika kata hiyo ili wauze mahindi hapo hapo.
“Nitaawagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri waje hapa Jumamosi hii na kufanya mkutano ili wawaeleze wana mpango gani kuhusiana na ujenzi wa soko hilo,” alisema.
Awali, mkazi wa kata hiyo, Ali Athumani, alimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili wajengewe soko la kimataifa kwa sababu wao ni wazalishaji wakubwa wa mahindi, lakini hawafaidiki nayo kwa sababu yote huuzwa katika soko la Kibaigwa mkoani Morogoro.
Naye Said Shabani, alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kufuatilia upatikanaji wa gari la wagonjwa na ujenzi wa wodi nyingine ya wagonjwa pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti kwenye zahanati yao.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu, amewaagiza viongozi wa serikali za vijiji kuanzia sasa kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yao.
Alitoa agizo hilo jana katika kijiji cha Engusero wilayani Kiteto, baada ya kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mji wa Kibaya.
Majaliwa alisema serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya na amewataka watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji kudhibiti suala hilo.
“Serikali haiwezi kuona vijana wanaangamia kwa dawa za kulevya. Tumeamua kudhibiti hali hiyo. Hii vita ni ya nchi nzima," alisema Waziri Mkuu.
“Tunataka vijiji vyetu, kata zetu, wilaya zetu na mikoa yetu iwe safi bila hata chembe ya dawa za kulevya.
"Tukikuona kijana unayumbayumba au kuweweseka, tunakupima na tukikuta umetumia ile kitu, tunakukamata ili utuambie ni nani amekupa.
“Sisi tunataka vijana wafanye kazi za kujiletea maendeleo. Kijana hawezi kuwa na maendeleo wakati hufanyi kazi, huwezi kuwa na ndoto za maendeleo wakati umelewa bangi au dawa za kulevya.
"Kila mmoja afanye kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA