Hivi Ndivyo Madini Aliyoshtukia JPM Yanavyosakwa Duniani


WAKATI Rais John Magufuli akikazia msimamo wa kuzuia usafirishaji nje ya nchi makontena ya mchanga wa dhahabu (makinikia), imebainika kuwa baadhi ya madini yaliyotajwa kuwamo katika mchanga huo, yanasakwa kwa udi na uvumba kutokana na umuhimu wake kiuchumi.

Aidha, imebainika kuwa mataifa yaliyopiga hatua kubwa kiuchumi kwa kuzalisha bidhaa za kielektroniki kama China na Japan, hutegemea madini hayo katika uzalishaji wa bidhaa kama simu za mkononi, kompyuta, DVD, vifaa vya ndege, betri za magari, satelaiti na hadi utengenezaji wa vinu vya nyuklia.

Jumatano iliyopita, Rais Magufuli alipokea ripoti kutoka kwa kamati teule aliyoiunda kuchunguza kila kilichomo katika makontena 277 yaliyoshikiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam ili mwishowe kulinda mapato ya nchi. Matokeo ya ripoti hiyo, iliyowasilishwa na mwenyekiti wake, Prof. Abdulkarim Mruma, yalionyesha kuwa kwa ujumla, thamani ya madini yote yaliyokutwa ni Sh. bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na Sh. trilioni 1.44 kwa kutumia viwango vya juu.

Kwa mujibu wa kamati, kiasi hicho cha fedha ni jumla ya thamani ya madini ya dhahabu, shaba na mengine ya metali mkakati (strategic metals) yaliyokuwa hayarekodiwi kabisa na kudaiwa kuinyima serikali mapato. Madini hayo ya mkakati yalitajwa kuwa pamoja na Sulfur, Iridium, Rhodium, Ytterbium, Beryllium, Tantalum na Lithium,Katika uchunguzi wa Nipashe uliohusisha rejea za taarifa mbalimbali kuhusu metali mkakati, imebainika kuwa madini ya jamii hiyo yana umuhimu mkubwa kwa sasa duniani na ndiyo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuiinua China kiuchumi.

Katika taarifa mojawapo iliyowahi kuchapishwa na jarida la Asia Times, toleo la Novemba 24 mwaka jana, ilionyesha kuwa ni madini ya jamii hiyo ndiyo yanayotumiwa na  China kama silaha kubwa ya vita ya kiuchumi dhidi ya mahasimu wao Marekani walio chini ya Rais Donald Trump na pia Japan, wakitumia kete ya kutishia kutowauzia madini hayo au kuyauza kwa bei ya juu.

Aidha, kwa mujibu wa gazeti la The Telegraph, toleo la Jumapili ya Machi 21 mwaka huu, China ndiyo kinara wa kuzalisha metaliki mkakati, wakishikilia asilimia 97 ya soko lote duniani.

Marekani, Japan na mataifa mengine yaliyoendelea hutumia madini hayo kwa matumizi mbalimbali yakiwamo pia ya kutengeneza vifaa vya udhibiti wa makombora na rada.

Akizungumza na Nipashe jana, Mhandisi wa Madini ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Karim Baruti, alisema metali mkakati zilizotajwa na kamati ya Prof. Mruma zina faida nyingi, ikiwamo kwenye utengenezaji wa vifaa vya elektroniki, mbolea na hata dawa.

MATUMIZI YA METALI MKAKATIWakati akielezea matumizi ya kila metaliki mkakati iliyotajwa na kamati ya kina Mruma, Dk. Baruti alisema Sulfur ndio chanzo kikuu cha ‘sulphuric acid’, inayotumika kutengeneza aina zote za mbolea ya sulfate (ammonium na potash) na pia hutumika kupunguza nyongo ya udongo aridhini kwa ustawi wa mazao. Pia hutumika kutengeneza madawa mbalimbali yakiwamo ya kuangamiza fangasi.

Kuhusu Rhodium, Dk. Baruti alisema kazi yake mojawapo ni kutengenezea vifaa mbalimbali vyenye uwezo wa kustahimili joto kubwa kama kwenye injini za ndege.

Dk. Baruti alisema madini ya Iridium huchanganywa na madini ya Platnum ili kuyaongezea nguvu yaweze kutumika kwenye mazingira ya joto kali na pia yakichanganywa na Osmium, hutengeza ncha ya kalamu na kompasi (compass bearings).

Akielezea baadhi ya matumizi ya madini ya Tantalum, Dk. Baruti alisema ni pamoja na kutengeneza vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta, simu za mkononi, seti za televisheni na vifaa vingine vya aina hiyo.

Aidha, Dk. Baruti alisema madini ya Lithium hutumika kutengeneza betri za simu za mkononi, vilainishi vya magari na pia hutumika kwenye viwanda vya kutengeneza vioo na katika uzalishaji wa madini mengine ya aluminum.

Kuhusu madini ya Ytterbiaum,  alisema baadhi ya matumizi yake ni pamoja na kutengenezea mashine za X-ray.

Madini ya Beryllium yana matumizi mengi muhimu kwa dunia ya sasa pia ikiwamo kutumika katika vipimo vya X-rays, utengenezaji wa ndege, satelaiti, vifaa vya kuzuia milipuko na pia katika vinu vya mionzi ya nyuklia.

Chapisha Maoni

0 Maoni