Je, unapenda kula udongo? Hii inakuhusu, tafadhali isome


MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Marc Rein mkoani Kigoma, Dk. Peter Mayengo amewashauri wajawazito kuacha kula udongo maarufu kwa jina la Pemba kwa kuwa ni hatari kwa afya zao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Mayengo alisema udongo huo ni hatari kwa afya kwa kuwa husababisha kuugua minyoo, kidole tumbo na magonjwa mengine   kutokana na chembechembe za mchanga na mayai ya minyoo.


Alisema wanawake kutumia udongo huo hasa wanapokuwa wajawazito   husababishwa na upungufu wa madini chuma   hatua ambayo huwasukuma kutafuta madini hayo na kuangukia kula udongo huo.

“Udongo huu una madhara makubwa   ambayo mara nyingi huonekana baadaye.

“Mjamzito anapaswa kuhudhuria kliniki   aweze kupatiwa dawa za kuongeza madini joto na kupata tiba ya magonjwa mengine anayopata katika kipindi hicho.

"Mjamzito akihudhuria kliniki   aweze kujifungua katika hali ya usalama anatakiwa kupata kinga ya magonjwa mengine kumkinga motto.

“Kwa utalaamu unapotumia udongo huu hauko salama kwa vile una bacteria na mayai ya minyoo na inaweza kusababisha mtumiaji kupata mikwaruzo katika utumbo wake,” alisema.

Diana John mkazi wa Kigoma Ujiji, alisema Pemba umekuwa kama ulevi kwake hususan kipindi cha ujauzito amekuwa akijikuta anakula udongo huo.

Alisema  kwa siku moja huweza kutumia vipande sita  na asipotumia anakuwa kama mgonjwa.

Alisema endapo kuna dawa   ambayo akila itamsaidia kuacha kula udongo huo yupo tayari kuitumia kuepuka madhara yanayosemwa na watalaam na akashauri itolewe   elimu.

Mfanyabiashara ya udongo huo, Mwamvua Ibrahimu, alisema udongo huo huchimbwa katika Kijiji cha Kitambuka mpakani mwa Burundi na Tanzania.

Alisema unatengeneza kwa kutumia maji na kuukanyanga ulainike ili kuunda katika vipande vidogo.

Alisema kwa siku moja  amekuwa akitengeneza magunia mawili ambayo kila gunia huliuza kwa Sh 9,000 na wateja  wakubwa ni wafanyabisahara wa mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Ibrahimu alisema udongo huo hupimwa na maofisa wa madini na wamekuwa wakitoza ushuru wa serikali.

Alishauri iwapo kuna madhara serikali ijiridhishe kwa kufanya utafiti wa kina

Chapisha Maoni

0 Maoni