Klabu ya soka ya wekundu wa msimbazi ya simba imetwaa ubingwa wa kombe la shirikisho la TFF baada ya jioni ya leo kuinyuka Mbao FC bao 2-1 kwenye mechi ya fainali iliyopigwa kunako dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.
Katika fainali hiyo iliyokuwa na ushindani wa hali ya juu, timu zote mbili zimepata mabao haoyo katika 30 zilizoongezwa kufuatia dakika 90 za kawaida kumalizika kwa timu zote kutoka nguvu sawa pasipo kufungana.
Alikuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Simba Fredrick Blagnon aliyeifungia Simba bao la kwanza dakika ya 108 kabla ya Mbao kusawazisha kupitia Robert Ndaki dakika ya 108 zikiwa zimesalia dakika 12 mchezo kuelekea katika changamoto za mikwaju ya penati.
bao hilo la Mbao lilitokana na mabadiliko ambayo kocha wake aliyafanya katika dakika za mwisho kwa kuwaingiza Rakesh Kotecha na Robert Ndaki wakati Mbao ikiwa nyuma, na kuiwezesha kuongeza mashambulizi ya nguvu langoni mwa Simba hadi bao hilo lilipopatikana na uzembe wa mabeki wa Simba waliodhani mfungaji ameotea, na kumuacha pekee yeye na golikipa Dan Agyei.
Ramadhani Shiza Kichuya akafunga bao la pili na la ushindi kwa Simba kwa penati baada ya mwamuzi kuamua adhabu hiyo iliyozua utata kwa madai kuwa beki wa Mbao aliunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Wachezaji wa Mbao walitaka kuigomea penati hiyo huku wakimzonga mwamuzi na kusababisha purukushani iliyodumu kwa takriban dakika 2, na kisha penati hiyo kupigwa katika dakika ya 120, ambapo hadi kipyenga cha mwisho, Simba 2, Mbao 1.
James Kotei wa Simba ameibuka mchezaji bora wa mchezo wa leo ambapo alionesha uwezo mkubwa katika safu ya ulinzi ya Simba kwa kudhibiti vilivyo kasi ya washambuliaji wa Mbao FC, huku Obrey Chirwa akiibuka mfungaji Bora wa michuano hiyo.
Mchezaji Bora wa Ligi Kuu msimu huu Mohamed Hussein alilazimika kutolewa nje mwanzoni kabisa mwa kipindi cha pili kutokana na maumivu aliyoyapata ambapo nafasi yake ilizibwa vilivyo na Abdi Banda
Kwa ushindi huo Simba imejinyakulia milioni 50 na kujikatia tiketi ya kucheza kunako michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu msimu wa mwaka 2012/13, huku mshindi wa pili akiambulia patupu zaidi ya medali kwa kuwa hakuna zawadi ya fedha kwa mshindi wa pili wa michuano hiyo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA