MJENGONI: Mdee awakalia kooni wabunge wa CCM

Mbunge  wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amewatibua wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuwashangaa jinsi wanavyoisifu Serikali kutokana na kufuta tozo, kodi na ada katika sekta za uvuvi, kilimo na mifugo.

Tukio hilo lilitokea bungeni jana wakati wabunge walipokuwa wakiendelea na mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Charles Tizeba.

Katika maelezo yake, Mdee aliwaambia wabunge hao kwamba pongezi zao katika kuondoa tozo hizo hazitakiwi kutolewa kwa kuwa wakulima hawajandaliwa mazingira mazuri ya kuwanufaisha na kilimo.

Kwa mujibu wa Mdee, sekta ya kilimo nchini inayohusisha asilimia 65 ya Watanzania, imekuwa ikishuka kila mwaka badala ya kupanda.

“Nashangaa sana waziri anasimama hapa na kutumia robo tatu ya hotuba yake kueleza masuala ya tozo,” alisema na kuongeza:

“Nawashangaa pia wabunge wanaosimama na kupongeza kuondolewa kwa tozo na naamini hizi pongezi zisingekuwapo kama Serikali ingekuwa imeandaa mazingira mazuri kwa wakulima hao.

“Nimesoma bajeti ya Waziri wa Viwanda, ameeleza kuna viwanda 234 vimesajiliwa kuanza, lakini viwanda vyote viko Dar es Salaam.

“Kwa tafasiri nyingine ni kwamba wabunge wa Kanda ya Ziwa ambao wanatoka katika maeneo ya kilimo cha pamba, bajeti hii haikuwaangalia kabisa ingawa mnasimama hapa na kupongeza.

“Kwa hiyo, napenda niwashauri wabunge wa CCM ambao ni wapya katika Bunge hili, kwamba kazi yetu ni kuisaidia Serikali na tunapokuwa tunatoa pongezi za aina hii wakati tukijua hali ni mbaya, tunaharibu nchi.

“Lazima wabunge wa CCM msome ilani ya chama chenu ambayo hata mimi wa chama cha upinzani huwa naisoma ili kupata maarifa na kujua jinsi mlivyojipanga.”

Pamoja na hayo, Mdee aliishutumu Serikali kwa kushindwa kutoa taarifa ya upimaji wa ardhi nchi nzima baada ya hoja yake kuungwa mkono na Bunge mwaka 2011.

Kutokana na maneno hayo, baadhi ya wabunge wa CCM walilazimika kusimama kwa nyakati tofauti na kuomba kumpa taarifa mbunge huyo.

Aliyekuwa wa kwanza kutoa taarifa ni Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, ambaye alimkosoa kwa kusema wabunge wote ni wapya kwa kuwa walipatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Mwingine aliyesimama ni Mbunge wa Nyasa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya, aliyesema kuipongeza Serikali baada ya kufuta tozo hizo ni jambo la msingi kwa sababu wabunge wanajua jinsi zilivyokuwa zikiwaumiza wakulima.

Kwa upande wake, Mbunge wa Newala, George Mkuchika, alimwambia mbunge huyo kwamba kila mbunge ana uhuru wa kupongeza katika eneo analoona kuna haja ya kufanya hivyo.

Wakati hao wakisema hayo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisimama na kumwomba Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, amlinde Mdee kwa kuwa anachokizungumza kinatokana na vitabu vya Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Chenge aliwataka wabunge wasiendelee kutoa taarifa kwa kuwa mwenye jukumu la kufafanua utendaji wa Serikali ni waziri mwenye dhamana.

“Kuna utaratibu mmeuanzisha hapa wa mbunge kusimama na kuomba kutoa taarifa na anayepewa taarifa hata kama ni nzuri, anaikataa.

“Lakini eleweni kwamba anayechangia hapa ni Mdee ambaye maelezo yake yanatakiwa kujibiwa na waziri mwenye dhamana,” alisema Chenge.

Juzi Dk. Tizeba wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema Serikali imefuta tozo, kodi na ada 108 zilizokuwa kero katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo.

Chapisha Maoni

0 Maoni