MKUU mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, ametakiwa kutoa kauli kuhusu wapi alipo Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane, ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 18, mwaka jana.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam.
Katambi ambaye alizungumzia kuhusu vitendo vya utekaji, ubambikaji kesi na uvunjaji wa haki za binadamu, alisema Jeshi la Polisi liko kimya juu ya taarifa za wapi alipo Saanane.
“Mnakumbuka majibu ya Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alipoulizwa kuhusu alipo Ben alitafuna maneno, hali iliyoonyesha anajua nini kinaendelea kuhusu Ben. Bavicha tunamtaka IGP mpya Sirro kutoa kauli ya Jeshi la Polisi kuhusu wapi aliko Ben, hasa kwa kuwa aliahidi kuwa vitendo vya kihalifu vitakoma na tunamtaka aanze na hili la Ben,” alisema.
Katambi pia alisema IGP Sirro anapaswa kubadili mfumo wa utendaji wa jeshi hilo, ili kuondoa uonevu dhidi ya raia, kuminya uhuru wa maoni, kukamata na kubambikia kesi raia wasio na hatia.
Alisema vijana wengi wanadhalilika kwa kukamatwa, hasa wa Chadema na kwamba katika mwendelezo huo, hata Yeriko Nyerere alikamatwa na watu wasiojulikana.
Katambi alisema yeye mwenyewe aliwahi kutekwa na watu wasiojulikana mara mbili, ikiwapo mwaka wa Uchaguzi Mkuu 2015, hivyo anashindwa kuelewa hadi imtokee nani ndipo hatua zichukuliwe.
“Tunazungumza ili hatua stahiki zichukuliwe, ikishindikana tutachukua hatua na sheria mikononi kumtafuta Ben Saanane,” alisema Katambi.
Akizungumzi suala la kutolewa silaha hadharani, alisema limeshawatokea baadhi ya viongozi waliokuwa serikalini, hivyo IGP Sirro ana wajibu mkubwa wa kusimamia utawala wa sheria.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA