Mwaka mmoja baada ya kifo cha aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Upinzani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Etienne Tshisekedi wa Mulumba, mwili wake haujarejeshwa nchini humo kwa ajili ya kuzikwa.
Etienne Tshisekedi alifariki February 1, 2017 katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels. Kutokana na kukosekana kwa makubaliano kati ya chama cha UDPS na serikali mjini Kinshasa, mwili wa Tshisekedi bado upo katika chumba cha kuhifadhi maiti mjini Brussels.
Kwa upande wa kambi ya Tshisekedi mjini Brussels, kipaumbele cha kwanza ni kurejeshwa kwa mwili wa Waziri Mkuu wa zamani nchini DRC, ambako anapaswa kuzikwa, katika moja ya sehemu ya familia yake katika eneo la N’Sele, mjini Kinshasa. Familia tayari imelipa Euro 16,000 kwa ajili ya kuendelea kuhifadhiwa kwa mwili wa Tshisekedi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Brussels.
Mitch Katumba, kiongozi wa chama cha UDPS mjini Brussels, amekua akikutana na viongozi wa Ubelgiji, Ufaransa pamoja na Ulaya, ili kuwezesha kurejeshwa kwa mwili wake nchini DRC. Mpaka sasa jambo hilo halijawezekana.
“Kabila, haipaswi kuwa na hofu, sio mwili wa Tshisekedi ambao utamuondoa madarakani, hakuna hoja yoyote kwa Tshisekedi kuzikwa nje ya nchi, Tshisekedi atazikwa DRC, katika mji wa Kinshasa. Tutajitahidi kusafirisha mwili wake,” -Katumba
“Sisi ni Waafrika, na sisi ni watu kutoka jamii ya Bantu. Kuna desturi, tuna maadili yetu. Mjane hawezi kukaa hivyo kwa mwaka mzima, wakati ambapo hatujamzika mumewe … Yuko hapo, analala chini, anaumia, ni mgonjwa, “ -Katumba.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA