Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amemtaka Waziri wa Katiba wa Sheria na Katiba Prof. Paramagamba Kabudi kubeba hoja yake binafsi aliyowasilisha Bungeni siku za hivi karibuni ili kuweza kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya chaguzi zijazo.
Kubenea ametoa kauli hiyo leo (Machi 11, 2018) wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kusema lengo la yeye kupeleka hoja binafsi ni kutokana na kutokuwepo kwa tume huru itakayoweza kujiendesha yenyewe mambo yake bila ya kutegemea kupata msaada serikali huku akitolea mfano suala la bajeti la kuendesha tume wakati wa chaguzi.
"Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lijadili na kuazimia serikali ipeleke Bungeni mswada wa marekebisho ya Katiba ili kuruhusu kuundwa kwa chombo huru kitakachoweza kusimamia uchaguzi kitachoitwa Tume Huru ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania", amesema Kubenea.
Pamoja na hayo, Kubenea ameendelea kwa kusema "suala la tume huru ya uchaguzi ni kilio cha watu wengi sana wakiwemo viongozi wa serikali, asasi za kiraia na vyama vya kisiasa. Kwa hiyo ni matarajio yangu kuwa watu wote wenye mapenzi mema na nchi hii wataungana na mimi na kuunga mkono hoja yangu na hivyo taifa taifa hili litaweza kupata tume huru kabla ya uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2020.
"Tume iliyoongozwa na Jaji Warioba ambayo Prof. Kabudi alikuwa kamishna ilileta mapendekezo ya kuwepo tume huru ya uchaguzi. Leo Prof. Paramaganda Kabudi ndiyo Waziri wa Sheria na Katiba wa serikali ya Rais Dkt. John Magufuli, ni matarajio yangu Prof. Kabudi atabeba hoja yangu kwa nguvu zote kuishawishi serikali, wabunge wenzetu waikubali na ije na maadhimio hayo".
Kwa upande mwingine, Kubenea amesema ni matarajio yake Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai atatumia busara zake zote na mamlaka aliyopewa ili kuruhusu hoja aliyoipeleka Bungeni ipite na izae matunda mazuri ndani yake.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA